INADAIWA kuwa chanzo cha Simba kufanya vibaya katika mechi za Ligi Kuu ni ukali wa kocha pamoja na ukata.
Simba imekuwa haina mwenendo mzuri tangu kuanza kwa mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu, na juzi ilifungwa mabao 3-2 na JKT Ruvu, matokeo
yaliyowashangaza wengi hasa kwa vile Ruvu ilifungwa mabao 6-0 dhidi
Prisons katika mechi iliyopita.
Habari za uhakika kutoka kwa wachezaji wa Simba ambao hawakutaka
majina yao yaandikwe gazetini zinadai kuwa, kocha Zdravko Logarusic
tangu kupewa timu hiyo amekuwa mkali kwa wachezaji na asiyetaka
kusikiliza ushauri wa benchi lake la ufundi.
Matokeo ya Simba ya juzi, imewafanya kuwa kwenye wakati mgumu katika
kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, kwani endapo hali itaendelea
hivi katika mechi zilizosalia, inaweza isiambulie kitu.
“Sio siri hatukupenda kufungwa na Ruvu, lakini kiukweli wachezaji
hatuna morali, tunacheza tu kwa vile tumesajili timu hii,” alisema mmoja
wa wachezaji hao.
“Unajua lazima tuseme ukweli, uongozi hautulipi maslahi yetu,
tumekuwa watu wa kuishi kwa kubangaiza, ukija uwanjani napo kocha
anakufokea kama mtoto mdogo, morali hiyo utaitoa wapi mchezaji?” Alihoji
mchezaji huyo.
“Kocha amekuwa mtu wa kutugombeza kila kukicha, bila kujua kama
wachezaji wake tunaishi
kwenye mazingira magumu, yeye akifika uwanjani
ukikosea kidogo anagomba tu, anatufanya kama watoto wadogo wakati sisi
ni watu wazima mpira ndio ajira yetu, kwanini tufanya makosa makusudi,
mambo mengine ni bahati mbaya tu,” alisema mchezaji mwingine.
“Na ukumbuke kuwa kocha huyo hatugombezi peke yake, anatutolea hadi
lugha ya matusi, kiukweli kabisa timu yetu haina morali,” alisema.
Aidha, wachezaji hao wamelalamika kitendo cha kocha kuwaweka nje
baadhi ya wachezaji kama Betram Mombeki na Issa Rashind ambao walikuwa
msaada mkubwa kwa timu, lakini tangu amefika Logarusic anaona wachezaji
hao hawafai.
“Halafu huyu ni kocha gani ambaye hataki ushauri wa wasaidizi wake?
Sasa wapo kwenye timu kwa ajili gani? Hata kwenye kufanya mabadiliko
ukimwambia usimtoe huyu anasaidia timu, yeye anafanya anavyojua yeye,
hakukuwa na maana basi awe na wasaidizi kumbe yeye mwenyewe anaweza
kwanini alipewa wasaidizi,” alihoji mchezaji mwingine wa timu hiyo.
Aidha, wachezaji hao walisema ukata nao unachangia kuwashusha morali,
kwani kwa sasa hawapati malipo yao inavyotakiwa na pia hakuna posho
zozote kwao.
“Unajua timu hizi mara nyingine zinakuwa na watu wake wa karibu
kusaidia, sasa Simba tulikuwa nao Friends of Simba hawa walikuwa
wakiisaidia sana timu hata inapokuwa na shida kifedha, lakini wale sasa
hawapo kwenye timu, mwisho hatumuoni kiongozi yeyote kuja hata
kuzungumza nasi kambini na kusikiliza matatizo yetu,” alisema mchezaji
mwingine.
“Sasa mwisho unakuta tupo kama mayatima, timu ikienda kucheza mikoani
posho zetu zinachelewa, mara nyingine unatoka Morogoro unakwenda Tanga,
mnafika huko ile posho ya Morogoro hamjalipwa wakati na sisi tuna
familia zetu hivyo tunashindwa kutekeleza majukumu yetu,” alisema.
Gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage azungumzie
hilo, lakini alisema atafutwe Katibu Mkuu Ezekiel Kamwaga kwa vile yeye
yupo bungeni Dodoma.
Hata hivyo Kamwaga hakupatikana kuzungumzia hilo baada ya simu yake
ya mkononi kuita bila majibu, hali kama hiyo ilitokea kwa msemaji wa
Simba Asha Muhaji ambaye simu yake haikupatikana karibu kutwa nzima ya
jana.
>>>HABARI LEO
No comments:
Post a Comment