Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, ameitaka Serikali kutoa
majibu sahihi baada ya gazeti la Daily Mail on Sunday la Uingereza,
kuchapisha habari inayoeleza kuwa Tanzania ni kinara wa ujangili, huku
Rais Jakaya Kikwete akifumbia macho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mchungaji
Msigwa alisema maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu baada ya kuchapishwa kwa taarifa hizo yamejaa siasa,
uzushi na uongo.
Alisema ukweli lazima uwekwe wazi kwa sababu
wanaohusika na biashara hiyo ni baadhi ya watendaji wa Serikali,
wafanyabiashara na vigogo wa vikosi vya ulinzi na usalama nchini.
Wakati Mchungaji Msigwa akieleza hayo, Ikulu ya
Marekani jana ilitoa taarifa ya kupiga marufuku biashara ya meno ya
tembo nchini humo ikiwa ni hatua yake ya kukabiliana na ujangili
ulioshika kasi katika nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Pia, leo Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa
viongozi 50 watakaohudhuria mkutano wa kuokoa viumbe vilivyo hatarini
kutoweka duniani, unaofanyika London, Uingereza.
Mkutano huo utakuwa chini ya wenyeji wa mwana wa Wales na Waziri wa Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Taarifa ya gazeti hilo ya Februari 8 mwaka huu,
limeitaja Tanzania kama kinara wa ujangili kwa kuua zaidi ya tembo
11,000 kwa mwaka na kumhusisha Rais Kikwete kuwa na urafiki na
wafanyabiashara ya meno ya tembo.
Pia imewahusisha wafadhili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika biashara hiyo.
Katika maelezo yake Mchungaji Msigwa alisema,
“Takwimu za Serikali zinaeleza wazi mwaka 2010 tembo 10,000 waliuawa
nchini sawa na wastani wa tembo 37 kwa siku. Inakuwaje taarifa hizi
ziwekwe wazi halafu Serikali idai inachafuliwa.”
Alisema Serikali imewahi kukiri kuwa inawajua
wanaojihusisha na ujangili lakini badala ya kuwakamata imekuwa ikiwataka
kuachana na biashara hiyo.
“Inakuwaje mtu anayevunja sheria za nchi
hakamatwi. Waziri Nyalandu amekuwa mlalamikaji badala ya kutafuta
suluhu, majibu yake na ya Serikali ya CCM yanadhihirisha kuwa mtandao
huu unaogopwa unaihusisha Ikulu, wanasiasa, polisi, maofisa wanyamapori
na wanajeshi,” alisema.
Msigwa alisema ni jambo la kushangaza kuona kuwa
hadi sasa Serikali haijawakamata watu wanaouza meno ya tembo ambao
wameonekana katika makala ya uchunguzi iliyorushwa na Kituo cha
Televisheni cha ITV cha Uingereza.
>>Mwananchi
>>Mwananchi
No comments:
Post a Comment