Wanachama wa Chadema wakikimbia huku wakiwa wamembeba Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchugaji Peter Msigwa mara baada ya kupatiwa dhamana na Mahakama
ya Wilaya ya Iringa jana. Picha na Said Ngamilo
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Iringa. Wakati Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimedai kufanyiwa hujuma, Mbunge wa
Iringa Mjini kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa amekuwa mbunge
wa pili kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kujeruhi.
Msigwa alifikishwa jana katika Mahakama ya Wilaya
ya Iringa akidaiwa kutenda kosa hilo juzi kwa kumjeruhi kada wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Salum Kaita kwenye mikutano ya kampeni ya kumnadi
mgombea wa udiwani wa Chadema katika Kata ya Nduli, Ayub Mwenda.
Juzi, katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Mbunge
wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi na wenzake 15, walipandishwa
kizimbani kwa tuhuma za kuwajeruhi wafuasi watano wa CCM katika kampeni
za udiwani na kulazwa rumande. Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema alijisalimisha polisi kutokana na taarifa za
kutafutwa kwake kutokana na tuhuma zinazohusiana na uharibifu wa mali
katika kampeni za udiwani. Aliachiwa baadae.
Mashtaka ya Msigwa
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa mahakama hiyo Godfrey Isaya, Wakili wa Serikali, Elizaberth
Swai alidai kuwa mnamo Februari 5 mwaka huu katika Kata ya Nduli, Msigwa
alimjeruhi Kaita kinyume cha sheria sura ya 12 ya mwaka 2002 kifungu
cha 225 cha kanuni ya adhabu.
Mchungaji Msigwa alikana mashtaka hayo na kuachiwa
kwa dhamana ya Sh2 milioni iliyowekwa na Mbunge wa Viti Maalumu
(Chadema), Chiku Abwao na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Lilian
Msomba.
Chadema walia na polisi
Kutokana na matukio hayo, Mkurugenzi wa Mafunzo na
Oganaizesheni wa Chadema, Kigaila Benson aliwaeleza waandishi wa habari
jana kuwa Jeshi la Polisi linatakiwa kuwatia nguvuni wale wote ambao
wanahusika na vitendo kuwajeruhi wanachama wao badala ya kupindisha
ukweli.
Akizungumzia vurugu zinazoendelea katika kampeni
za kuwania udiwani kwenye kata 27, Kigaila alisema uongozi wa CCM na
Polisi kwa pamoja wanajua kinachotokea lakini wanakifumbia macho.
“Watu wetu wanajeruhiwa, wanakamatwa wanawekwa
mahabusu na tunapotoa taarifa polisi hazichukuliwi hatua. Inakuaje watu
wanaoumiza watu wetu hawakamatwi? Polisi wanatakiwa kuzingatia sheria na
kanuni kwa wote,” alisema Benson.
Kasulumbayi apata dhamana
Mahakama ya Wilaya ya Kahama jana mchana
ilimwachia kwa dhamana Kasulumbayi aliyekuwa ameshikiliwa kwa tuhuma za
kuwacharanga mapanga wafuasi wa CCM kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani
wilayani Kahama.
No comments:
Post a Comment