NA NYEMO MALECELA
VYAMA vya michezo iliyoshiriki michuano ya Jumuiya Madola vimesema
endapo ripoti ya meneja wa timu ya Tanzania, Mwarami Mchume haitabainisha
ukweli wa yale yaliyojitokeza katika michuano hiyo, vitatoboa siri kwa
Watanzania.
Wakizungumza na SWACOTZ FORUM jana kwa nyakati tofauti viongozi wa vyama vya
michezo hiyo, walisema wanasubiri ripoti ya Mwarami ili waweze kupasua jipu na
endapo haitasema ukweli basi wao wataungana na kuitisha mkutano utakaoleza
ukweli wa yale yaliyotokea.
Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Ruta Rwakatale
alisema wao tayari wameongea na mabondia walioshiriki michuano hiyo ambapo
wameoanisha maelezo yao na ripoti ya kocha Jonasi Mwakipesile aliyeambatana nao
na kujua sababu zilizopelekea kushindwa kupata medali.
“Tunasubiri ripoti ya meneja wa timu, ikitofautiana na yale tuliyoelezwa
na kocha na mabondia tutaeleza ukweli maana tunayo mambo mengi yaliyosababisha
tukose medali kwani pointi walizozipata mabondia wetu zinaonyesha ni kiasi gani
tuliwaandaa vizuri,” alisema.
Nao makocha wa judo, Zaidi Hamisi, Ramadhan Namkoveka (kuogelea) na
Ramadhan Othman (mpira wa meza) wamesema wanasubiri ripoti hiyo ili waeleze
ukweli.
“Tunasisitiza ripoti ya meneja inatakiwa ieleze ukweli maana kuna mambo
mengi yaliyosababisha sisi kushindwa kufanya vizuri na endapo itaficha chochote
sisi tutaeleza ukweli ili Serikali itambue kuwa viongozi wa wizara ya michezo wameshindwa kuwajibika,” alisema.
No comments:
Post a Comment