EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Monday, May 26, 2014

MKURUGENZI WA TANESCO APANDISHWA KIZIMBANI KWA UBADHILIFU WA MAMILIONI YA FEDHA ZA UMMA


Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando (kushoto), akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es SalaamALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando na mkewe Eva Mhando, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na makosa mbalimbali, likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kughushi.
Mbali na Mhando na mkewe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea, Jamhuri Johnson, ni Francis Machalange (Mhasibu Mkuu Tanesco), Sophia Misidai (Mhasibu Mkuu) na Naftali Kisinga, ambaye ni ofisa ugavi wa shirika hilo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai shitaka la kwanza linamkabili Mhando pekee ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Ilidaiwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 31 mwaka 2011, Tanesco Makao Makuu, Mhando akiwa mwajiriwa, kwa makusudi alishindwa kutaja maslahi yake kuhusiana na Kampuni ya Santa Clara, ambayo wakurugenzi wake ni mke wake, Eva na watoto wake, kitendo ambacho kilisababisha kampuni hiyo kupewa mkataba wa kusambaza vifaa vya ofisi kwa Tanesco vyenye thamani sh milioni 884.5.
Mwendesha mashitaka alidai kutokana na hali hiyo alikiuka maadili ya Tanesco na sheria ya uongozi wa maadili ya umma na kusababisha kampuni hiyo kupata faida isiyo halali ya sh milioni 31.7.
Wakili wa Swai alidai shitaka la pili ambalo linamkabili Eva ni kughushi; kwamba kati ya Januari 6 na Julai 30 mwaka 2011 katika sehemu zisizojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa dhamira alighushi ripoti ya ukaguzi wa mahesabu iliyoonyesha Kampuni ya Finx Capital House iliifanyia ukaguzi Kampuni ya Sant Clara mwaka 2010, jambo alilokuwa akijua ni uongo.
Katika shitaka la tatu ambalo ni la kughushi linalomkabili Eva, ilidaiwa kati ya Agosti 9 mwaka 2011, jijini Dar es Salaam, alighushi hati ya kuhamisha hisa kwa lengo la kuonyesha kwamba alihamisha hisa zake 200 zenye thamani ya sh 10,000 kwenye Kampuni ya Sant Clara kwa Eveta John Shing’oma, huku akijua ni uongo.
Aliendelea kudai kuwa shitaka la nne ambalo linamkabili Eva ni la kuwasilisha nyaraka za uongo kinyume cha sheria Makao Makuu ya Tanesco, kwamba Agosti 5 mwaka 2011, aliwasilisha taarifa ya fedha ya kampuni ya Sant Clara kwa Katibu wa Bodi ya Zabuni ya Tanesco, ambayo ilionyesha ripoti hiyo ya fedha iliandaliwa na Finx Capital Houes huku akijua ni uongo.
Katika shitaka la tano, ilidaiwa kwa njia ya udanganyifu kati ya Aprili Mosi na Oktoba 31 mwaka 2011, Eva akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Sant Clara, alijipatia sh milioni 31.7 kutoka Tanesco kupitia usambazi wa vifaa vya ofisi baada ya kuwasilisha nyaraka za uongo ambazo ni ripoti ya ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2007/2008 na orodha ya mikutano mikubwa ya miaka miwili.
Shitaka la sita linawakabili Francis Mchalange, Sophia Misidai na Naftali Kisinga ambalo ni la matumizi mabaya ya madaraka.

Kwamba Oktoba 17 mwaka 2011, katika Makao Makuu ya Tanesco, wakiwa ni waajiriwa wa shirika hilo kama wahasibu wakuu na ofisa ugavi, kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kutoa maelezo ya uongo kwa lengo la kuonyesha Sant Clara ni kampuni bora na ina vigezo ambavyo ilistahili kupewa zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi vya Tanesco.
Washitakiwa wote walikana tuhuma hizo mbele ya Hakimu Moshi ambaye alimtaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi ya sh milioni nane kila mmoja. Pia mshitakiwa hataruhusiwa kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali.
Washitakiwa hao walitimiza masharti hayo, na kesi imeahirishwa hadi Juni 13 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
SOURCE>>>TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment