MWENYEKITI
mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taaluma za Juu Tanzania (TAHLISO),
Amon Chakushemeire, amesema jumuiya hiyo inaendeshwa kitaaluma na si
kisiasa.
Chakushemeire aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam wakati wa
kukabidhi nafasi hiyo kwa mwenyekiti mpya wa TAHLISO, Moses Mdee, na
kueleza kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kuacha kuitumia jumuiya hiyo
kwa lengo la kujinufaisha.
Alisema kuwa wapo baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuwania nafasi za juu
za uongozi wamekuwa wakiingilia majukumu ya kiuongozi ya jumuiya hiyo.
“Wapo wanasiasa wanaotarajia kugombea urais mwaka 2015 wanaingilia
uongozi wa TAHLISO kwa utashi wao ili iendeshwe kisiasa, hali
iliyosababisha kutaka kuingiza usiasa na kutuletea wagombea wao katika
uchaguzi uliofanyika mwaka jana,” alisema.
Chakushemeire alisema licha ya jumuiya hiyo kutegemea taasisi za nje
katika kujiendesha, lakini katiba yao hairuhusu kushirikishwa wanasiasa
ikiwemo kusaidiwa na taasisi zinazojiendesha kisiasa.
Alisema changamoto inayoikabili TAHLISO ni wimbi la wanafunzi wa
elimu ya juu kugubikwa na siasa badala ya kuweka malengo katika elimu
itakayowanufaisha kwa maisha yao ya baaadae.
“Ni jambo la kusikitisha kuona elimu yetu sasa ni uwanja wa siasa,
wanasiasa wengi wanawatumia wanafunzi wa elimu ya juu kujinufaisha
kisiasa ikiwa ni pamoja na kupiga kampeni za siri siri,” alisema.
SOURCE: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment