Akizungumza
na Tanzania Daima juzi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John
Mnyika, amekitaja kikundi cha Green Guard kuwa cha hatari kutokana na
kuhusika na matukio mengi ya kigaidi.
Mnyika
amesema matukio hayo yana baraka zote za CCM na serikali kutokana na
ukweli kwamba kikundi hicho hakiguswi wala kuchukuliwa hatua na vyombo
vya dola, pamoja na kuhusishwa kwa ushahidi mwingi na matukio mengi.
“Hawa
wameshiriki matendo mabaya ya utekaji, upigaji, kujeruhi na yapo ya
vifo. Lakini kwa sababu kinafanya haya kwa baraka za CCM na serikali
yake, hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya yeyote.
“Tumetoa
taarifa nyingi tu na zenye ushahidi wa waziwazi wa kuhusika kwa kikundi
hicho, ambacho sasa kinasimamiwa na Mwigulu Nchemba, lakini polisi hao
hao wanaotusakama leo kwa vile tumeamua kusema ukweli, hawajachukua
hatua zozote dhidi ya yeyote yule,” alisema Mnyika.
Aliongeza
kuwa CHADEMA imesema sana kuhusu ukatili huo, lakini katika hali ya
kusikitisha viongozi wa siasa wanaojitokeza kulaani hatua ya chama hicho
kuamua kutoa mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake, wamegeuka mabubu
kuikemea CCM na serikali yake.
Malalamiko
hayo ya CHADEMA yanafanana pia na yale yaliyotolewa juzi katika ripoti
ya Shirika la Konrad Adenauer Stiftung la Ujerumani linalojihusisha na
utafiti wa masuala ya siasa nchini.
Shirika hilo
katika ripoti yake ambayo inadaiwa kusambazwa ndani na nje ya nchi,
imeshutumu vikali matukio hayo, huku ikisukuma lawama kwa vyombo vya
dola kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaodaiwa
kuhusika na ukatili huo.
Pia shirika
hilo limetahadharisha kuwepo kwa uwezekano mkubwa zaidi wa vitendo vya
kikatili kwa viongozi wa vyama vya upinzani, wanaharakati na wakosoaji
wa serikali kadiri chaguzi zinavyokaribia.
Ripoti hiyo
iliyoandikwa na Danja Bergman na Stefan Reith, iliyotolewa tangu mwezi
uliopita, inazungumzia matukio mbalimbali yaliyolikumba taifa kwa siku
za karibuni, yakiwemo ya mabomu yaliyolipuliwa katika mkutano wa CHADEMA
na Kanisa Katoliki la Olasiti jijini Arusha.
Hata hivyo,
wachunguzi hao wana maoni kuwa ongezeko la matumizi ya mabavu kutoka kwa
vyombo vya dola dhidi ya maandamano halali na ukosoaji, ni dalili tu ya
mambo makubwa zaidi yanayoweza kutokea katika kipindi cha miaka miwili
ijayo, ambayo uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unatarajiwa
kufanyika.
Ripoti hiyo
pia inasema katika hali hiyo, kwa kadiri ya hali ilivyo kila aina ya
vitisho, udanganyifu na matumizi ya mabavu vitakuwa vikibadilishwa
badilishwa na kutokea katika sura tofauti ikiwemo vurugu ili kupotosha
umma, huku watuhumiwa wakishindwa kutambuliwa, na wale wanaotambuliwa
watafichwa au kutochukuliwa hatua zozote za kisheria na mamlaka husika.
Ripoti hiyo
imeenda mbali zaidi na kusema kuwa hata pale vyombo vya dola
vinapohusishwa na mauaji, kwa ushahidi wa wazi, watuhumiwa wamekuwa
wakilindwa na kuendelea kutesa mitaani bila kuchukuliwa hatua zozote za
kisheria, badala yake wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakishitakiwa kwa
kesi mbalimbali za kubambikiza, zikiwemo uchochezi, ugaidi na
kuhamasisha chuki kati ya wananchi na serikali yao.
CHADEMA imeorodhesha matukio yanayodaiwa kutendwa na vijana wa CCM kama ifuatavyo:
Juni 16 na
Julai 14 katika uchaguzi wa kata nne za Arusha vurugu nyingi
ziliripotiwa zikiwahusu wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi kuteka, kujeruhi
na kupewa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kusimamia shughuli za ulinzi
katika chama hicho kikongwe nchini.
No comments:
Post a Comment