EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, June 27, 2013

HABARI ZA MICHEZO KWA KINA........

WEBBER AAMUA KUACHANA NA LANGALANGA MWISHONI MWA MSIMU.

DEREVA nyota wa langalanga wa timu ya Red Bull, Mark Webber ameamua kuachana na mashindano hayo ikifikapo mwishoni mwa msimu huu. Katika miaka 12 ambayo amekuwa akishiriki michuano ya langalanga Webber ambaye pia amewahi kuendesha katika timu za Minard, Jaguar na Williams ameshinda mashindano mbalimbali ya Grand Prix mara tisa na kumaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano ya dunia mara tatu. Akihojiwa kuhusiana na uamuzi huo Webber amedai kuwa anadhani huo ni wakati muafaka kwake kuachana na mbio za langalanga na kuangalia mambo mengine. Msimu wake mzuri ulikuwa ni mwaka 2010 ambapo aliongoza karibu msimu wote kabla ya kuteleleza katika mashindano matatu ya mwisho na kushuhudia dereva mwenzake wa Red Bull Sebastian Vettel na Fernando Alonso wa Ferrari wakimpita. Dereva wa Lotus Kim Raikkonen ambaye ni bingwa wa michuano ya dunia mwaka 2007 ndio anapewa nafasi kubwa kuchukua nafasi ya Webber ambaye aliingia katika langalanga mwaka 2002.


TEVES ATUA JUVENTUS.

KLABU ya Juventus ya Italia jana ilimtangaza rasmi kumsajili mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez kutoka timu ya Manchester City kwa mkataba wa miaka mitatu. Taarifa zinadai kuwa klabu yenye maskani yake katika jiji la Turin wamelipa kiasi cha paundi milioni 10 kwa nyota huyo mwenye umri wamiaka 29. Lakini Tevez atatakiwa kumaliza adhabu yake ya kutumikia jamii kwa saa 250 ili kuondoka jijini London salama na kuepuka kuburuzwa tena mahakamani. Tevez alikatisha likizo yake huko Amerika Kusini na kupanda ndege kuelekea Italia jana lakini pia atatakiwa kumaliza adhabu yake aliyopewa na mahakama ya Macclefield April mwaka huu kwa kuendesha huku akiwa amefungiwa kufanya hivyo.

KIRUI, KIPSANG WAJITOA MARATHON MOSCOW.

BINGWA mara mbili wa dunia mashindano ya mbio ndefu Abel Kirui na mshindi wa medali ya shaba katika michuano ya olimpiki Wilson Kipsang wamejitoa katika timu ya wanariadha ya Kenya itakayoshiriki michuano ya riadha ya dunia itakayofanyika jijini Moscow. Makamu wa rais wa Chama cha Riadha cha nchi hiyo Paul Mutwii amedai kuwa Kurui aliwafahamisha kwamba amejitoa kwasababu ya kusumbuliwa na majeraha wakati Kipsang yeye amewaambia kuwa ana majukumu mengine. Kirui ambaye alishinda taji la dunia la mbio ndefu mwaka 2009 na 2011 amekuwa akisumbuliwa jeraha la kifundo cha mguu wake wa kulia na anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita. Kuziba nafasi hizo Mutwii amesema wamewaita Mike Kipyego ambaye alishinda mbio za marathon jijini Tokyo mwaka jana, Bernard Kipyego mshindi wa medali ya fedha mbio za nusu marathon 2009 na bingwa wa mbio za marathoni za Paris Peter Some. Kikosi cha mwisho kitakachokwenda Moscow kitatajwa mwezi ujao baada ya kufanyika mbioza mchujo.

BADO SIJAFULIA - FEDERER.

MCHEZAJI tenisi nyota wa Switzerland, Roger Federer amesisitiza kuwa bado ataendelea kucheza mchezo huo kwa miaka mingi ijayo pamoja na kutolewa mapema katika michuano ya Wimbledon jana. Nyota huyo ambaye anashika namba tatu katika orodha za ubora duniani amesema hana hofu yoyote pamoja na kutolewa na Sergiy Stakhovisky wa Ukraine katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Katika mchezo huo Federer aliburuzwa kwa kufungwa 6-7 7-6 7-5 7-6 na Stakhovsky anayeshika namba 116 katika orodha za ubora duniani. Baadhi ya wadau wa mchezo huo wamekuwa wakihoji kiwango cha Federer mwenye umri wa miaka 31 na kudai kuwa amekwisha lakini mwenye amesisitiza kuwa bado yuko fiti na ataendelea kucheza kwa miaka kadhaa ijayo. Kwa upande wa wanawake mwanadada nyota anayeshika namba mbili kwa ubora kwa upande wanawake Maria Sharapova wa Urusi naye aliyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha 6-3 6-4 kutoka kwa Michelle Larcher de Brito wa Ureno anayeshika namba 131 katika orodha hizo.

BADO HATUKO FITI KWA KOMBE LA DUNIA - SCOLARI.

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luis Felipe Scolari amekiri kuwa kikosi chake bado hakiwezi kuanza kuota kunyakuwa taji lao la sita la Kombe la Dunia mwaka ujao lakini wamebakisha mechi moja kunyakuwa taji lao la tatu la Kombe la Shirikisho baada ya kuiengua Uruguay katika hatua ya nusu fainali. Scolari amesema anafikiri kikosi hicho kimefikia mahali pazuri lakini bado kuna vitu vingi vya kufanyia marekebisho mpaka kikamilike kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa wanahamishia nguvu zao katika mchezo wa fainali na baada ya hapo wataangalia mapungufu yalijitokeza ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kitakachoweza kulibakisha Kombe la Dunia nyumbani. Brazil kwasasa wanasubiri mshindi wa nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itakayopigwa baadae leo kati ya mabingwa wa Ulaya na Dunia Hispania watakaochuana na Italia.

Wednesday, June 26, 2013

RONALDO AZIDI KUWATIA TUMBO JOTO MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo anaweza kuwa njiani kurejea Manchester United kutokana na tetesi kuwa atafanya mazungumzo na viongozi wa Old Traford katika siku tatu zijazo. Nyota huyo wa klabu ya Real Madrid amekuwa akihusishwa na tetesi za kurejea Uingereza baada ya kuonekana kukosa furaha huko Santiago Bernabeu lakini inaaminika kwamba ujio wa Carlo Ancelotti unaweza kushawishi kubakia nchini Hispania. Gazeti moja nchini Hispania liliripoti kuwa Ronaldo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Ureno atakutana na viongozi hao wa United kabla ya kurejea Madrid kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi. Meneja mstaafu wa United Sir Alex Ferguson katika kipindi cha karibuni amekuwa akimfukuzia Ronaldo ambaye inaaminika kutaka nafasi ya kuiwakilisha klabu hiyo ambayo ndiyo iliyomtengeneza mpaka kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani. Rais wa Madrid Florentino Perez amenyesha kuwa na uhakika wa nyota huyo mwenye thamani ya paundi milioni 80 kusaini mkataba mwingine ambao utambakisha nchini humo lakini Ronaldo alikanusha habari hizo katika mitandao ya kijamii.

NEYMAR HAWEZI KUMFUNIKA MESSI BARCELONA - SYLVINHO.

BEKI wa zamani wa klabu ya Barcelona, Sylvinho anaamini kuwa Neymar atapata wakati mgumu wa kumfunika Lionel Messi kufuatia uhamisho wake kutoka klabu ya Santos kwenda kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Hispania. Mambo makubwa yanategemewa ka mshambuliaji huyo nyota wa kimataifa wa Brazil kufuatia kiwango bora anachokionyesha katika michuano ya Kombe la Shirikisho lakini Sylvinho anafikiri Neymar mwenye miaka 21 anaweza kuishia kucheza nyuma ya Messi kwenye klabu hiyo. Sylvinho anakiri kuwa Neymar ni mchezaji wa wachezaji bora kabisa kwasasa lakini suala la kumfunika Messi ambaye ameshinda tuzo nne za Ballon d’Or litakuwa suala gumu sana. Beki huyo aliendelea kusema kuwa kumekuwa na wachezaji wengi nyota wa Brazil kama Ronaldo, Romario na Ronaldinho lakini wote hao hawajapata kufikia kiwango alichonacho Messi kwasasa. Sylvinho amewahi kushinda mataji matatu ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona katika kipindi cha kuanzia mwaka 2004 mpaka 2009.

No comments:

Post a Comment