EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Thursday, July 10, 2014

RAIS KIKWETE AMTOLEA UVIVU JANUARY MAKAMBA



Mbunge huyo wa Bumbuli, ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, alitangaza uamuzi huo akiwa Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye kufafanua nia hiyo katika mahojiano na gazeti hili.PICHA|MAKTABA 
Tanga. Rais Jakaya Kikwete amezungumzia nia ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kutaka kuwania urais mwakani, akisema mwanasiasa huyo kijana “anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha”.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kutoa maoni yake kuhusu wanachama wa CCM wanaotaka kuwania urais, baada ya chama hicho kuwaonya makada sita kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kutaka nafasi hiyo kubwa.
Akiwa jijini London, Makamba alitangaza nia yake ya kuwania urais mwaka 2015, akisema huu ni wakati wa fikra mpya ambazo zinahitaji vijana na kwamba wazee wakae kando.

Jana, Rais Kikwete, ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Soni Bumbuli mkoani Tanga anakoendelea na ziara ya siku tano, alimtaka Makamba “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka.
“Nasikia kuwa bwana mdogo January anataka mambo makubwa. Mie hajaniambia, na mie nasikia. Hata alipogombea ubunge hakuniambia nilisikia baadaye... asilazimishe, wakati ukifika atapata, na akikosa asilete nongwa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alitoa mfano wake mwenyewe aliposhindwa katika uteuzi wa mgombea urais wa CCM mwaka 1995, wakati akiwa na miaka 45 (miaka minne zaidi ya umri wa Makamba ifikapo 2015), akisema kuwa hakukata tamaa na aliendelea kusikiliza ushauri wa wazee hadi alipofanikiwa kukalia nafasi hiyo ya juu mwaka 2005.
Mwenyekiti huyo wa CCM, ambaye pia ushawishi wake unaweza kuamua mteule wa chama, alimtaka mbunge huyo wa Bumbuli asikilize ushauri wa wazee.
Pamoja na ushauri huo kwa mwandishi wake wa zamani wa hotuba, Rais Kikwete alimpongeza kwa kazi nzuri ya ubunge jimboni humo na akaeleza kuwa anamsaidia katika wizara yake.
Alinukuu maneno ya aliyekuwa katibu mkuu wa Afro Shiraz na swahiba wake, Thabit Kombo aliyemwambia Kikwete kuwa “wakati ukifika utapata”, hasa kutokana na kiu yake ya muda mrefu ya kuwatumikia Watanzania.
“Nilipokosa mwaka 1995 sikukata tamaa, ndipo 2005 nikaingia, na huo ndio ulikuwa wakati wangu wa kushika wadhifa huu. Wakati ukifika watu watake wasitake utakuwa wewe tu,” alisema Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja takriban wiki moja baada ya Makamba kueleza nia yake ya kuwania urais akisema kwa asilimia 90 ameshaamua kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Mbunge huyo wa Bumbuli, ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, alitangaza uamuzi huo akiwa Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye kufafanua nia hiyo katika mahojiano na gazeti hili.

No comments:

Post a Comment