“Hakuna lolote humu ni blabla tu… Mheshimiwa Zambi wewe ulikuwa
‘backbencher’ (kiti cha nyuma) kama mimi ulikuwa unapiga muziki kama
kasuku juu ya wizara hii, leo unashirikiana na waziri wako unakuja na
vitu ambavyo havina majibu, maana yake nini?”.PICHA|MAKTABA
Dodoma. Mbunge machachari wa
Mwibara, Alphaxard Kangi Lugola, amedai kuwa Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii.
Lugola ambaye katika Bunge lililopita aliwaongoza
wabunge wenzake kuichachafya Serikali hadi mawaziri wanne kujiuzulu
nyadhifa zao, jana aligeuka tena mwiba kwa Serikali ya CCM.
Akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika, Lugola alisema anashangaa Waziri mwenye dhamana, Christopher
Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blabla.
Pia alimgeukia naibu wa wizara hiyo, Godfrey Zambi
na kumwambia kuwa amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma
bungeni akipaza sauti, lakini baada ya kupata madaraka amewageuka na
kushirikiana na waziri.
Akichangia kwa hisia kali, Lugola alihoji
inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za
umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki ofisini
kama Waziri.
“Waziri huyuhuyu ndiye anayezindua mbegu aina ya
Chutoni ambayo haioti, bado ni Waziri. Waziri huyu huyu analipa ruzuku
mbegu ya pamba isiyoota bado ni Waziri,” alisema Lugola.
Lugola alihoji kama Mchina aliyekuwa akijenga
daraja la Kilombero alijiua kwa sababu tu ya kuhofia kupigwa risasi
atakaporudi kwao, hata Waziri Chizza alipaswa awe ameiacha kazi hiyo.
“Simshauri waziri ajiue, lakini kwa vitendo vyote
hivi waziri huyu angekuwa ameacha wizara hii na kupumzika na kufanya
kazi nyingine mbadala,” alisema Lugola huku akipigiwa makofi.
Lugola alikumbushia Chizza alikuwa ni miongoni mwa
mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo na kusema mambo yanayofanywa na
wizara hiyo yatakigharimu Chama Cha Mapinduzi.
Mbunge huyo alibainisha kuwa, katika hotuba yake
mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Serikali iko kwenye
mchakato wa kuanzisha mfuko wa kinga ya pamba ili kuwasaidia wakulima.
Hata hivyo, alisema katika hotuba ya Waziri Mkuu
juzi, hakuna sehemu aliyozungumzia mfuko huo wala Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika katika hotuba yake ya mwaka huu, naye hajazungumzia
mfuko huo.
“Hivi nchi hii tunaiendesha kwa usanii mpaka lini?
Usanii juu ya usanii… Hatuwezi kuwadanganya wananchi kwa kiwango hiki.
Itakuwaje mimi mbunge niunge mkono bajeti ya namna hii?” alihoji.SOURCE>>>MWANANCHI
No comments:
Post a Comment