Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais
wa SMZ, Maalim Seif Sharif Hamad wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo
yao nyumbani kwa Karume, Mbweni mjini Zanzibar. Na Mpigapicha Wetu
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa viongozi
hao wamekutana faragha Aprili 30, nyumbani kwa Rais huyo mstaafu eneo
la Mbweni mjini Unguja.
Viongozi wengine walioshiriki mazungumzo hayo ni
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mkurugenzi
wa Uenezi, Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo na
Katibu Mtendaji wa Kamati hiyo, Mansoor Yussuf Himid.
Wajumbe wengine katika msafara huo walikuwa ni
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu na Eddy Riyami huku mjumbe
mmoja wa kamati hiyo, Aboubakary Khamis Bakary ambaye ni Waziri wa
Katiba na Sheria wa (SMZ) akikosekana.
Imeelezwa kuwa kamati hiyo ilitoa muhtasari wa
mwelekeo wa mjadala wa Katiba Mpya na sababu za wajumbe wa Ukawa
kutoshiriki vikao vya Bunge la Katiba.
Kamati hiyo ilitaja ni Bunge hilo kutawaliwa na
ushabiki, vijembe, matusi na kebehi, huku ikielezwa pia kuwapo na
dhamira ya kupuuzwa maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba kupitia Rasimu
ya Pili ya Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Mzee Moyo
aliithibitishia jana kamati yake kukutana na Rais mstaafu Karume, ingawa
alikataa kuelezea lolote lililojadiliwa wala kutaja azimio lililofikiwa
baada ya kikao hicho kumalizika.
“Ni kweli kamati yangu ilikutana Rais Mstaafu
Karume nyumbani kwake, wala si kificho, tumekubaliana Jussa atakuwa
ndiye mzungumzaji wa yale tuliyoyazungumza na kuafikiwa, yeye na
Mansoor ndiyo makatibu watendaji wa kamati yetu,”alisema Mzee Moyo.
Gazeti hili lilipompigia simu Rais Mstaafu Karume ili aeleze ajenda na madhumuni ya kikao hicho, hakuwa tayari kueleza lolote.
Hata hivyo, baada ya kumalizika mkutano huo,
baadhi ya viongozi hao akiwamo Maalim Seif , Jussa na Mzee Moyo
walikwenda moja kwa moja kushiriki mkutano wa hadhara wa Ukawa
uliohutubiwa na viongozi wa juu wa CUF, NRA, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi
na NLD.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF,
ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa
akizungumza na Mwananchi Jumapili amesema kwamba walikutana na Rais
Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume kama waanzilishi wa maridhiano ya
kupatikana kwa mwafaka wa kisiasa Zanzibar na hatimaye kuunda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema katika mkutano wao na Rais Mstaafu Karume,
walizungumza kuhusu jinsi ya kulinda maridhiano na Serikali ya Umoja wa
Kitaifa hasa kutokana na kuwapo baadhi ya watu wenye mwelekeo wa kutaka
kuvuruga maridhiano hayo.SOURCE>>>MWANANCHI
No comments:
Post a Comment