Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Nape Nnauye
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na
Michael Matemanga
Dar es Salaam. Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kimesisitiza msimamo wake wa kutaka kuendelea na muundo
wa Serikali mbili huku kikiweka wazi kuwa kina masilahi makubwa na
mfumo huo.
Kimesema suluhisho la kumaliza changamoto za
Muungano siyo kubadili muundo wake na kuwa na Serikali tatu, bali ni
kuufanyia maboresho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema: “Kimsingi CCM
ndiyo waasisi wa Muungano na ina masilahi makubwa na mapana na Muungano
huu kama waasisi pengine kuliko taasisi nyingi ndani na nje ya nchi
yetu.”
Alisema licha ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kueleza bungeni sababu za Tume hiyo
kupendekeza mfumo wa Serikali Tatu, chama hicho kinaamini kuwa suluhisho
la kero za Muungano haziwezi kumalizwa kwa kubadili muundo wake.
“Kazi ya Warioba na Tume yake sasa imekwisha
rasmi. Kwisha kwa kazi yao ni mwanzo wa awamu nyingine ya mchakato huu.
Mwisho wa kazi ya tume hiyo siyo mwisho wa mjadala juu ya Katiba
tuitakayo, bali ni mwanzo wa awamu nyingine mbili za mjadala mpana na
maboresho kama siyo marekebisho ya kuondoa upungufu kwenye rasimu
iliyowasilishwa. Awamu hizo mbili ni Bunge la Katiba na Kura ya Maoni.”
Alisema katika Bunge la Katiba kutakuwa na fursa
nzuri ya kupima kama yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na maelezo ya
ziada yaliyotolewa na Jaji Warioba yanaakisi maoni ya Watanzania walio
wengi.
“Tuna imani na awamu mbili zilizobaki kwa kuwa
zinahusisha wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge Maalumu la Katiba na
nyingine kuwahusisha wananchi moja kwa moja, zitatumika vizuri kutupa
jibu la nini matakwa ya Watanzania juu ya Katiba waitakayo,” alisema
Nape.
Alisema chama hicho kinatambua umuhimu wa
kuimarisha Muungano na kwamba njia pekee ya kuudumisha ni kufanya
maboresho kwenye muundo wa Serikali mbili.
Akitolea mfano kero za Muungano, Nape alisema:
“Hivi sasa tuna Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ambayo ni ya Muungano. Moja ya malalamiko ya Zanzibar ni kwamba katika
Serikali ya Muungano kuna baadhi ya mambo siyo ya Muungano ni ya
Zanzibar.” Aliongeza: “Lakini unapozungumzia misaada na mikopo kutoka
nje lazima ipitie kwenye dhana inayoitwa uhusiano wa kimataifa. Wao
wanasema wizara ambazo siyo za Muungano zinakosa fursa ya kupata misaada
na mikopo kutoka nje kwa sababu hazipo katika Muungano na hazifanyi
kazi na wizara za Muungano.”
Alisema suluhisho la jambo hilo siyo Serikali
tatu, bali ni kutenganisha uhusiano wa kimataifa na mambo ya nje, “Mambo
ya nje mnaweza kulifanya kuwa la Muungano. Uhusiano wa kimataifa
mkalitenga. Kila upande utakuwa na uhuru wa kuwa na uhusiano wake, hilo
linaweza kufanyika hata kukiwa na Serikali mbili.”>>>>MWANANCHI
No comments:
Post a Comment