Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali ya Kenya, Seneta Amos Wako
akizungumza jana, wakati wa Semina ya Bunge Maalumu la Katiba. Picha na
Salim Shao
Dodoma. Mwanasheria Mkuu (AG)
mstaafu wa Kenya, Amos Wako amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
kutokupuuza maoni ya wananchi katika kutunga Katiba ya nchi vinginevyo
watazua mgogoro.
Wako, ambaye kwa sasa ni Seneta wa Busia ya
Mashariki nchini Kenya, alitoa ushauri huo jana katika semina kwa
wajumbe wa Bunge la Katiba kuhusu uzoefu wa namna nchi hiyo ilivyopitia
misukosuko ya kuipata Katiba mpya.
Wako ambaye kwa miaka 21 alikuwa katika wadhifa wa
AG, alisema matukio mengi yaliyosababisha Kenya kutokupata Katiba yao
kwa wakati, yalitokana na kutokuwashirikisha wananchi moja kwa moja
katika mchakato.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 2: 11,
mwanasheria huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba ya Kenya
alionya pia kuwa Katiba inayotengenezwa hapa nchini isiwe ya kunukuu
kutoka katika mataifa mengine kwa sababu mahitaji yanatofautiana kwa
kila nchi.
“Katiba isiwe ya mazungumzo kutoka kwa viongozi
pale Dar es Salaam, kwani itakuwa ni mali ya watu wachache na ambayo
lazima itapingwa, hata sisi tulianza hivyo lakini tulishindwa vibaya,”
alionya Wako.
Aliimwagia sifa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa
bungeni Jumanne iliyopita, kwamba kwa mtindo ilivyowasilishwa inaonekana
kuwajali na kuwapa nafasi zaidi wananchi wa hali ya chini.
“Pamoja na hayo, lakini Katiba hii ikiingiliwa
zaidi na kutekwa na wanasiasa au kikundi cha watu wachache kwa masilahi
yao, inaweza kuharibika kama ilivyotokea kwetu Kenya ambako Kanu
walikuwa wakipinga kila kitu wakatufanya tuingie katika mgogoro.”
Alisema kuwa mitazamo ya wanasiasa huwa ni tatizo
na hatari katika kutafuta Katiba mpya na dawa pekee na ya maana ni kutoa
nafasi kwa wananchi waamue wenyewe.
“Mfumo uliowekwa katika mchakato wa kuunda Katiba
mpya nchini kwenu, kwamba Rasimu ya mwisho ya Katiba itoke bungeni na
kupelekwa moja kwa moja kwa wananchi ni mzuri, ni muhimu maoni ya
wananchi ya awali yazingatiwe,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Bunge Maalumu limeaminika kufanya kazi hiyo ili kuwasaidia wananchi kufikia malengo yao.
Uzoefu wa Kenya
Akizungumzia uzoefu wa Kenya katika kupata Katiba
mpya alisema walianza kwa kukabiliana na changamoto kubwa ya ukabila
ambayo kila jamii ilikuwa haiamini kundi jingine katika kutafuta usawa,
jambo alilosema ni tofauti na Tanzania.>>>>MWANANCHI
No comments:
Post a Comment