Dar es Salaam. Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii imesema kuwa takwimu zinaonyesha kwamba wanawake
20,000 nchini wanaishi na ugonjwa wa Fistula.
Hayo yamo katika hotuba ya Mke wa Rais, Salma
Kikwete aliyoitoa kwenye hafla iliyowakutanisha wanawake mashuhuri
nchini iliyofanyika Dar es Salaam.
“Licha ya ugonjwa wa fistula kutibika kirahisi,
kutokuwapo kwa ufahamu, umaskini na unyanyapaa vimekuwa ni kikwazo kwa
wengi kutibiwa,” alisema Mama Salma.
Salma aliipongeza Kampuni za Simu za Mkononi za
Vodacom na Hospitali ya CCBRT kwa kuwakomboa wanawake wenye ugonjwa huo.
A lisema kwa msaada wa kampuni hiyo na CCBRT, imepanua huduma zake kwa
kuongeza vituo vingine vya afya Tanzania na hivyo kuwafikia wanawake
wengi zaidi.
“Jamii za kimataifa zimegundua kuwa, kuna faida
kubwa kama tutaziba pengo la kijinsia lililopo katika masuala ya afya
kwa kuwapatia wanawake uhuru ili waweze kuishi maisha ya furaha,”
alisema.
Naye Mkuu wa Idara ya Vodacom Foundation, Laura
Turkington alisema tangu huduma ya ujumbe na matibabu yaani text to
treatment utambulishwe mwaka 2010, zaidi ya wanawake 1,900 wamefaidika
na kufanyiwa operesheni ya fistula.
Alisema operesheni hiyo ilibadilisha maisha ya wanawake na waliweza kufanya kazi zao na kuishi maisha yenye furaha.
“Leo hii ninavyozungumza Taasisi ya CCBRT ni kituo
kikubwa duniani cha matibabu ya ugonjwa wa fistula, kwa misaada kutoka
kwa Serikali za Uswisi na Uholanzi pamoja na Kampuni ya Vodafone
Foundation,” alisema.
No comments:
Post a Comment