EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Tuesday, January 28, 2014

SERIKALI YAIBIWA BIL.3/- NA KAMPUNI YA ERONLINK

erolinkKAMPUNI ya Erolink imeiibia serikali kiasi cha sh bilioni tatu za mapato kutoka kwa waajiriwa wapya katika kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka, alisema wizara imefanya uchunguzi wa kina kuhusu wizi huo na kubaini kuwa utaratibu unaofanywa wa kukodisha wafanyakazi kwa baadhi ya wakala wa huduma binafsi unakiuka Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999 iliyorejewa mwaka 2002 sura ya 243.
Kabaka alisema uchunguzi huo umebaini ujanja wa kukwepa kodi na kujipatia faida kwa kukwepa kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu wa sheria za kazi.
Waziri huyo alisema kuna baadhi ya makampuni yamefanyiwa uhakiki na Mamlaka ya Mapato (TRA) na kubainika kukwepa kodi ya mshahara (PAYE) na kodi ya mapato ya kampuni kinyume cha kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya mwaka 2004 (sura ya 332 kama ilivyorejewa mwaka 2008).
Alitaja baadhi ya kampuni zilizobainika kukwepa kodi hiyo kuwa ni Omega Equipment and Job,
Tarent Man Power, Tanzania Breweries Ltd (TBL), Kalahar na Coast to Coast.
“Wizara ya Kazi na Ajira imeamua kusitisha mara moja utaratibu wa mawakala kuwaajiri wafanyakazi wanaowatafutia kazi, hivyo mawakala na kampuni husika waliopo kwenye utaratibu huo kwa sasa wanapaswa kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwa wakala kwenda kwa kampuni husika ndani ya mwezi mmoja kuanzia leo,” alisema.
Kabaka alisema uchunguzi unaendelea kufanyika kama kuna wafanyakazi wa kigeni wanaohusika katika utaratibu wa  kukodisha ili hatua zinazostahili zichukuliwe ikiwemo kuwataka waombe vibali vya ajira kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995 na Sheria ya huduma za ajira namba 9 ya mwaka 1999.
“Wizara ya Kazi na Ajira inawaeleza Wakala wa Huduma za Ajira nchini, kwa utaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za maombi ya usajili wa uwakala kwa Kamishna wa Kazi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Ajira namba 9 ya mwaka 1999 (sura 243 kama ilivyorejewa  mwaka 2002) ili wafanye shughuli za uwakala wa huduma za ajira kisheria,” alisema waziri huyo.
Alisema maombi hayo yawasilishwe katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya muda huo wakala asiye na kibali cha Kamishina wa Kazi hataruhusiwa kuendesha shughuli za huduma za ajira nchini.
>>>Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment