Mauaji ya kutisha yametikisha wilaya ya Tarime kiasi cha kumfanya Mkuu wa Jeshi
la Polisi (IGP), Ernest Mangu, kutuma timu maalum kutoka makao makuu ya jeshi
hilo inayohusisha kamisheni ya Operesheni kufanya uchunguzi.
Hatua
ya kupelekwa kwa timu hiyo inatokana na mauaji ya mfululizo katika mji wa
Tarime ambayo ipo kwenye himaya ya Kanda Maalum ya Polisi ya Tarime na Rorya
ambayo yametokea kwa watu wanane katika kipindi cha siku tatu.
Mauaji
hayo yanadaiwa kufanywa na jambazi mwenye silaha katika mji wa Tarime mkoani
Mara kwa siku tatu kuanzia Jumatatu hadi jana.
Mmoja
wa watu waliouawa ni askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Koplo Zakaria Chacha Mwita ambaye ni mtoto wa marehemu Meja Jenerali Mwita
Marwa.
Pia
wamo aliyekuwa Mhandisi Ujenzi Wilaya ya Rorya, aliyetajwa kwa jina la David
Mwasi Misiwa.
Wengine
ni mfanyabiashara, Samuel Richard Mohenga na huku Jeshi la Polisi likisema kuwa
linaendesha msako.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Royra, Justus Kamugisha, alithibitisha kutokea
kwa mauaji hayo na kusema kuwa mtu anayesadikiwa kuwa jambazi akiwa na bunduki
kwa siku tatu kuanzia Januari 26, mwaka huu usiku aliua watu saba kwa kuwapiga
risasi na kujeruhi kadhaa.
Aliwataja
wengine kuwa ni mwendesha bodaboda, mkazi wa kijiji cha Nkende, Juma Marwa
Nyaitara, Erick Lucas Makanya, mfanyabiashara wa bucha mkazi wa kijiji cha
Rebu, Juma Mwita Mroni na mkazi wa kijiji cha Kenyamanyori, Robert Chacha
Kisiri.
Jana
asubuhi, wakazi wa mji wa Tarime na vitongoji vyake walimfananisha mtu
aliyekuwa amevaa koti refu na mtuhumiwa wa mauaji hayo na kutaka kumshushia
kipigo, lakini aliokolewa na polisi waliorusha risasi hewani na kumpeleka
katika kituo cha polisi.
Kamanda
Kamugisha aliwashauri wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa
taarifa mara watakapomuona mtuhumiwa.
Alisema
polisi wanafanya msako katika vijiji vya Kenyamanyori, Rebu, Nkende, Mogabiri
na Kibumaye katika kata za Kitare, Turwa na Binagi kwenye Tarafa ya Inchage.
Mkuu
wa Mkoa wa Mara, John Tuppa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele
wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime jana
walitembelea maeneo ya vijiji ambavyo wakazi wake wameuawa na jambazi hilo.
TIMU YA MAKAO MAKUU
Alizungumzia
timu iliyotumwa Tarime, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi
nchini, Kamishna Paul Chagonja, alisema kuwa ni ya wapelelezi na Intelijensia
na inakwenda kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa na mkoa wa Mara
kuhakikisha jambazi huyo anakamatwa ili kuondoa hofu kwa wananchi.
Chagonja
alisema juhudi za kumsaka jambazi huyo zinaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi
kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
SOPHIA
SIMBA ALAANI MAUAJI
Wakati
huo huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, amelaani
maauji ya wanawake watano waliotaarifiwa kuuawa katika wilaya za Musoma,
Butiama na Rorya mkoani Mara.
Alisema
wizara inasisitiza kuwa mtazamo huo ni hasi na unakwenda kinyume cha haki za
binadamu hivyo jamii haina budi kuachana na imani zinazosababisha mauaji.
“Wizara
inahimiza wananchi kupinga dhana potofu zinazopelekea mauaji ya wanawake ikiwa
ni pamoja na imani za kishirikina, uchu wa kupata utajiri wa haraka, kulipiza
kisasi na kuendeleza hulka ya ukatili katika jamii,” alisema.
Alisema:
“Mauaji dhidi ya wanawake yanapotokea katika jamii zetu yanarudisha nyuma
juhudi za serikali katika kuzuia ukatili dhidi ya wanawake katika jamii
kutokana tu na tofauti za kimaumbile.
Wizara
inaitaka jamii itambue kuwa wanawake wana haki ya kuthaminiwa utu wao na
kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza kuhatarisha
haki yao ya kuishi ambayo ndiyo haki kuu kuliko haki zote,” alisema na
kuongeza:
“Kushamiri
kwa mauaji ya kikatili wanayofanyiwa wanawake katika wilaya za mkoa wa Mara ni
jambo ambalo linasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanawake. Mauaji hayo
yanawakosesha amani na utulivu na hivyo kuzorotesha ari yao katika shughuli za
uzalishaji mali.”
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment