![]() |
| MBUNGE WA JIMBO LA KAWE MH:HALIMA MDEE |
WAZIRI wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametakiwa
kujiuzulu kutokana na kuonyesha kupwaya katika nafasi yake na kushindwa
kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la Kapunga, wilayani Mbarali, mkoani
Mbeya.
Wiki
iliyopita Profesa Tibaijuka alidaiwa kuzomewa baada ya kuingia ndani ya
gari la mkuu wa wilaya na kufanya mazungumzo na mwekezaji aliyekuwepo
katika mgogoro na wananchi wanaogombania eneo la kijiji chao, kisha
aliposhuka akabadili msimamo wa awali wa kutetea haki na stahili za
wanakijiji hao na kugeuka kuanza kumtetea mwekezaji hapo hapo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana,
Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee,
alisema kushindwa kutatuliwa kwa mgogoro huo uliodumu kwa miaka mingi
sasa ni mwendelezo wa kushindwa kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kusimamia suala nyeti la ardhi na kudhihirisha kuwa Profesa
Tibaijuka amepwaya katika nafasi yake, hivyo hana budi kujiondoa.
Mdee alisema
kuzomewa kwa waziri huyo ni wazi kuwa mgogoro huo bado unafukuta na
unaonekana kuigharimu serikali ya CCM, pia imemjengea taswira mbaya ya
kisiasa Profesa Tibaijuka.
Alisema
Watanzania kutokana na migogoro ya ardhi ilipofikia anahitaji mtu makini
kwenye wizara hiyo ambaye anaweza kusema na kutenda bila kuonekana
akifanya vitendo vya gizani kama ilivyotokea hivi karibuni huko Kapunga.
“Tunataka
Waziri Tibaijuka awaambie Watanzania, mawaziri wanaoshindwa kama yeye
chini ya serikali isiyowajibika kutatua matatizo ya wananchi wanataka
yatokee maafa makubwa kiasi gani ili wajue kuwa migogoro ya ardhi
inaweza kulitumbukiza taifa kwenye sintofahamu?,” alihoji.
Mdee
alimtaka Profesa Tibaijuka kuacha kuanzisha jambo jipya katika mgogoro
huo ambapo itakuwa ni kinyume cha kauli ya serikali hiyo hiyo iliyowahi
kutolewa bungeni juu ya kushughulikia suala hilo.
Alisema kuwa
serikali kupitia kwa Waziri Christopher Chiza iliwahi kutoa
‘commitment’ bungeni tangu mwaka 2009 na 2011 kuwa ili kumaliza mgogoro
wa ardhi katika shamba la Kapunga, inamalizia taratibu za kurekebisha
hati ili mwekezaji abakie na eneo linalomstahili pekee.
“Pia
wanakijiji warudishiwe eneo lao la kijiji. Hiki ndicho ambacho
wanakijiji wale wanasubiri Profesa Tibaijuka atekeleze. Kinyume cha hapo
anadhihirisha kuwa serikali ilidanganya Bunge na wananchi,”
alisisitiza.
Alisema kuwa
wananchi hao wanajua serikali ilishatoa ahadi ya kuwarudishia eneo lao,
hivyo wanataka Profesa. Tibaijuka atekeleze kauli ya serikali badala ya
kuanza mchakato mpya kama vile suala hilo limeanza hivi karibuni.
“Si siri kwamba suala la migogoro ya ardhi limefika mahali pabaya. Watu wanauana… kwa silaha za kisasa na jadi,” alisema.
Alisema kuwa
iwapo waliopo madarakani, hususan katika wizara husika wangeguswa na
damu ya Watanzania ambayo imeanza kumwagika kwa sababu ya ardhi,
wasingeendelea kufanya ‘vituko’ kama alivyofanya Profesa Tibaijuka kwa
kushindwa kutekeleza msimamo wa serikali uliotolewa mbele ya wawakilishi
wa wananchi.
Alisema kuwa
serikali kupitia wizara husika iwaeleze Watanzania wanataka watu
wangapi wafe ili washtuke na kumaliza migogoro katika maeneo mbalimbali
ikiwamo Kiteteo, Kapunga, Mvomero, Mtibwa, Malinyi na Kilombero.
Alisema kuwa
kutokana na serikali kupuuza na kutochukua hatua za haraka, matokeo
yake yameanza kuonekana ikiwemo waziri huyo kuzomewa na wananchi
waliokerwa na kitendo chake cha kubadilisha msimamo wake na kumruhusu
mwekezaji kuendelea kumiliki eneo la ardhi katika shamba hilo.
Alisema kuwa
kutokana na nafasi aliyonayo Profesa Tibaijuka na kuujua ukweli ulivyo
katika chimbuko la mgogoro huo ambapo serikali yenyewe kupitia NAFCO
iliuza ardhi kwa mwekezaji (hekta 7,370) na kusajili na kupata hati
moja kwa eneo lote zikiwamo hekta 1,870 za kijiji.
“Tulitarajia
baada ya kuwa ameujua ukweli ulivyo angesimamia haki ionekane
ikitendeka kupitia kauli ya serikali bungeni kwamba mwekezaji akabidhi
hati yake serikalini ifanyiwe marekebisho, wanakijiji wapate stahili
yao,” alisema.
Alisema
kutokana na utaratibu ule ule wa utendaji kazi wa kizembe, wenye
viashiria vya rushwa, waziri hakuonekana kujali kauli hiyo, akapuuza
hata ile aliyoitoa mwenyewe mapema kwenye kikao na wananchi, kabla
hajapanda kwenye gari la mwekezaji akiwemo mkuu wa wilaya.
“Haya
yaliyotokea Kapunga ni sehemu ya matukio mengi yanayoihusisha serikali
kuuza ardhi kwa wawekezaji, wananchi wakiwa ndani ya ardhi hiyo! Tofauti
na watu wa Kapunga, ambao waliamua kufanya kitendo cha kijasiri cha
kumzomea waziri wakafikisha ujumbe wao,” alisema.

No comments:
Post a Comment