CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa sharti ambalo kama
halitatekelezwa chama hicho hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wala hakitapiga kura ya
kupitisha rasimu ya katiba.
Sharti
hilo lilitolewa mjini Bukoba juzi na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe,
wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo mikutano ya
Operesheni ya M4C Pamoja Daima uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa na
kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Alisema
chama hicho hakitashiriki uchaguzi iwapo Serikali haitaboresha Daftari la
Kudumu la Wapigakura wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu na upigaji kura wa
rasimu ya katiba.
Mbowe
alisema kwa jins hali inavyoonesha Serikali haioneshi nia ya kuboresha Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura wakati tunaelekea katika uchaguzi Mkuu mwakani.
Alisema
katika utafiti wao wamebaini kuwepo kwa vijana zaidi ya milioni 5.3 ambao
wamefikisha umri wa miaka 18 wanaotakiwa kushiriki kupiga kura mwakani kuchagua
viongozi wao.
Alisema
katika hilo nchi itasimama kwa vile kama tunahitaji mabadiliko hayawezi
kufanyika bila kuboresha daftari la kura. Kuhusu Rasimu ya Katiba, Mbowe aliapa
mbele ya mkutano huo kuwa mwaka huu ndio atang’olewa meno bungeni, kwani
hawatakuwa tayari kuburuzwa wakati wa Bunge la Katiba lijalo .
Alisema:“Suala
la katiba halina masihara ni maisha yenu, maisha ya watoto wenu, maisha ya
vizazi na vizazi, ni maisha ya taifa letu kila Mtanzania mwenye umri wa miaka
18 wa kupiga kura lazima apige kura kukubali rasimu ya katiba mpya, nasi
Bungeni hatutakubali kuburuzwa. ”
Alisema
kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kujadili rasimu
ya katiba mpya. Alisema bunge lijalo la katiba wao wanaenda kujadili rasimu ya
Katiba Mpya ambayo tayari wameshaona .
“Tayari
CCM wanampinga Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
kuhusiana na maoni ya wananchi kutaka serikali tatu, wakati wao haimo kwenye
sera yao, hapa kuna tatizo, kwani sisi tunaenda kujadili maoni yawananchi wengi
si kutetea sera za vyama vya siasa,” alisema.
Alisema
katiba si suala la kidini, sera za vyama vya siasa wala la kikabila , bali ni
ya watu wote kwa ajili ya mustakabali wa maisha na taifa kwa ujumla, hivyo
hawaendi Dodoma kwa ajili ya kupinga Katiba hiyo, bali kupitisha maoni ya
wananchi wanavyotaka.
Pamoja
na mambo mengi, Mbowe aliwapongeza madiwani wa Manispaa hiyo bila kujali
itikadi za vyama kuungana kupinga ufujaji wa kodi za wananchi maskini wa
Manispaa uliokuwa ukifanyika ndani ya Manispaa hiyo.
“Mimi
napenda kuwapongeza Madiwani wa Manispaa ya Bukoba pamoja na Mbunge wao, Balozi
Kagasheki, ambao kwa pamoja walisimama kutetea maslahi ya wananchi wa Bukoba,
ukweli tuuseme na mnyonge mnyongeni na haki yake mpeni,” alisema.
Wakati
huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA),Tundu Lissu, amewaonya baadhi ya wanasiasa wanaotumia makanisa na
misikiti kuwashawishi wananchi ili wawachague kuwa viongozi katika uchaguzi wa
mwaka huu 2014/15.
Lissu
aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza katika mikutano miwili iliyofanyika
katika Kijiji cha Ilongero na Mjini Singida juzi wakati akiwa kwenye siku ya
kwanza ya ziara ya ujumbe wa chama hicho ikiwa ni mwendelezo wa Operation M4C
Pamoja Daima itakayofanyika nchi nzima.
Alisema
kuwa pamekuwa na tabia ya baadhi ya wanasiasa Wakristo na Waislamu ambao hupita
makanisani na misikitini na kutoa fedha kwalengo la kujijengea umaarufu jambo
ambalo aliwataka wananchi wawe macho nao.
Alisema
pamoja na wanasiasa hao kujiwekea mazingira ya kushawishi wananchi ili
wawachague, Watanzania hawawakubali kwani hiyo inaweza kuleta tofauti za
kidini.
“
Lazima tukumbuke mafundisho ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere
ambayo yalisisitiza kuzingatia amani, upendo na mshikamano kwa kuepuka
kugawanywa na watu hao,” alisema.
Kuhusu
Katiba Rasimu ya Pili ya Katiba, alisema ni nzuri na kuzingatia vipengele vingi
vilivyotolewa maoni kurekebishwa kazi ambayo ilifanywa na CHADEMA pamoja na
wananchi wengine.
Alisema
suala kubwa ni kuona kuwa Rasimu hiyo haichakachuliwi kwa manufaa ya chama cha
siasa au viongozi kwa ajili ya maslahi yao.
“Tunasisitiza
kuwepo kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kuboreshwa ili
wananchi wengi wakiwemo vijana waliofikia umri huo na wale waliopoteza shahada
zao waweze kushiriki katika zoezi laku pigakura za maoni,”alisema.
Katika
hatua zingine , Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA Taifa, John Henje,
alisema chama hakitavumilia mtu yeyote anayetaka kukizamisha chama hicho. “Mtu
yeyote akileta mchezo atafukuzwa, CHADEMA itaendelea kwani hakuna aliye mkubwa
au maarufu kuliko wanachama,” alisema. Alieleza kuwa chama hicho kitaendelea
kuwepo na kinachotakiwa sasa ni kuzungumzia mambo ya msingi yanayokijenga na
kukiendeleza.
>>Gazeti la Majira.
.....

No comments:
Post a Comment