EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Monday, December 9, 2013

MJUE MANDELA NA MICHEZO


MANDELA AKIWA NA TIMU YA OLIMPIKI YA TANZANIA MWAKA 2000 MJINI SYDNEY, AUSTRALIA
“Jela si kuwa inachukua uhuru wako pekee, badala yake inachukua hata utambulisho wako wa wewe ni nani kwa kuwa kila mmoja anavaa sare, anakula chakula sawa na wengine na anafuata ratiba zilezile.

“Kwa kifupi ni wizi wa uhuru wa mhusika na kama mpigania uhuru na mwanaume wa shoka, kikubwa ni kupambana kwa nguvu zote na hali hiyo ambayo inaua au kupoteza muonekano wa uwezo wa watu husika.”
Maneno hayo yako mwanzo kabisa kinapoanza kitabu cha Long Walk To Freedom Volume 2 cha Nelson Mandela ambacho nilikinunua Mei 24, 2003 kwenye nyumba ya makumbusho ya Mandela iliyoko katika Mtaa wa Villakazi, Soweto jijini Johannesburg.
Ni miaka kumi na ushee sasa tangu wakati huo, tukiwa na watu wengine wachache tulipata kuonyeshwa vyombo, nguo, viatu na vitu vingine alivyokuwa akivitumia Mandela wakati akiishi katika nyumba hiyo na mkewe, Winnie Mandela.
Baadaye tukatembezwa kwenye nyumba ambayo alihamia Mandela na ile aliyokuwa akiishi mkewe wa zamani, Winnie Mandela. Pamoja na mengi makubwa aliyofanya Mandela, kwangu kilichonivutia zaidi kwake ni namna alivyoshiriki michezo.
Huenda wengi wameelezea, lakini ukiangalia picha zake zilizokuwa katika nyumba hiyo ya makumbusho zinaonyesha alikuwa ni mwanamichezo wa kweli, kwani si ngumi tu, mchezo uliojulikana kuwa kipenzi chake, lakini soka na kikapu pia alishiriki.
Kwangu naamini wanaoshiriki michezo wanaaminika kuwa binadamu wenye maamuzi ya haraka zaidi kuliko wengine, angalia mpira wa kikapu, soka na hata ngumi namna mtu mmoja ambavyo huamua vitu vingi kwa wakati mmoja kwa kuwa muda ni mchache na mambo mengi hutakiwa kufanyika katika kipindi kifupi.
Kwa Mandela hakuwa Mzungu, inaonekana imekuwa ni vigumu kwa Wazungu kutamka kuwa ndiye binadamu maarufu zaidi kuliko wengine wote duniani katika kipindi hiki.
Kifo chake, bado kinamfanya awe mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wengine wote duniani, hasa aliyeshiriki katika kupigania uhuru wa nchi fulani kwa muda mrefu zaidi na kusaidia kuiokoa nchi.
Baada ya kuwa rais mweusi wa kwanza wa Afrika Kusini, Mandela amekuwa ndiye kiongozi mwanasiasa maarufu zaidi na kipenzi cha wanamichezo kuliko wengine wote duniani.

Makocha maarufu, akiwemo Alex Ferguson, amewahi kueleza namna alivyofurahishwa na maisha au ushujaa wa Mandela, alimtembelea na kuonyesha furaha yake kwake wakati Manchester United ilipokuwa Afrika Kusini kwa mechi za kirafiki.
Tanzania:
Kuna mengi yanayoonyesha kuwa Mandela alikuwa na urafiki mkubwa na Tanzania, kwani hata alipokamatwa Agosti 5, 1962 na baadaye kuhukumiwa gerezani, inaelezwa alikuwa anatokea hapa nchini.
Lakini kwenye kitabu chake cha Long Walk To Freedom, kuna maneno kadhaa ya Kiswahili yaliyotumika, ikionyesha wazi namna alivyokuwa na mapenzi na nchi hii.
Moja ya picha kwenye kurasa hizi zinamuonyesha akiwa na timu ya taifa ya Olimpiki ya Tanzania ambayo alipiga nayo picha mwaka 2000.

JK ATOA CHANGAMOTO KWA UONGOZI MPYA TFF.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini. Ametoa changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania. Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa miguu nchini. “Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini. “Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini. “Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake. Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka, lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini. Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.

HAPATOSHI LIGI YA MABINGWA BARANI ULAYA.

WAKATI hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ikielekea mwishoni wiki hii timu kadhaa zitaungana na Manchester United, Real Madrid, Paris Saint-Germain, Bayern Munich, Manchester City, Chelsea, Atletico Madrid na Barcelona katika hatua ya timu 16 bora. Timu zilizopo kundi A na D zitacheza mechi zake za mwisho kesho wakati makundi mengine yaliyobakia yatacheza mechi zao Jumatatu huku timu kadhaa zikihitaji ushindi ili kusonga mbele katika michuano hiyo. Katika kundi A Shakhtar Donetsk wanaweza kukata tiketi ya kusonga mbele kama wakifanikiwa kuifunga Manchester United ugenini wakati sare inaweza pia kuwavusha kama Bayer Leverkusen ikishindwa kuifunga Real Sociedad. Kwa upande wa kundi D Juventus itajihakikishia kuendelea kuwepo katika michuano hiyo kama wakishinda au kutoa sare dhidi ya Galatasaray jijini Instabul wakati kwa upande mwingine Galatasaray watasonga mbele kama wakifanikiwa kuchukua alama zote tatu kutoka Juventus.

DROGBA, EBOUE MATATANI KWA KUONYESHA FULANA KUMKUMBUKA NELSON MANDELA.

KAMATI ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la Uturuki-TFF linatarajia kuwahoji nyota wawili wa kimataifa wa Ivory Coast wanaocheza klabu ya Galatasaray, Didier Drogba ba Emmanuel Eboue kufuatia kuonyesha ishara katika mechi ya kumkumbuka rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela aliyefariki dunia Alhamisi. Baada ya Galatasaray kushinda mabao 2-0 dhidi ya SB Elagizspor katika mchezo wa Kombe la Ligi Ijumaa, nyota hao wawili walivua fulana zao na kubakia na vesti zilizokuwa na ujumbe kuhusu Mandela. Mara baada ya Drgba kuvua fulana yake vesti aliyokuwa amevaa ndani ilikuwa na maandishi yaliyosema “Thank you Madiba” akimaanisha asante Madiba wakati vesti ya Eboue ilikuwa na maandishi yaliyosomeka “Rest in Peace Nelson Mandela” akimaanisha pumzika kwa amani Nelson Mandela. TFF linakataza kuonyesha fulana yoyote yenye ujumbe unaohusiana na mambo ya siasa wakari wa mechi ya soka.


WENGER ALIKATAA BAO LA KUSAWAZISHA LA EVERTON.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ameonyesha kutofurahishwa na bao la kusawazisha la Everton baada ya timu hiyo kushindwa kukaa kileleni kwa tofauti ya alama saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Bao la kusawazisha la Everton lililofungwa na Gerard Deulofeu katika dakika ya 84 liliifanya Everton kuchukua alama muhimu katika Uwanja wa Emirates baada ya pia ya kuwafunga Manchester United katikati ya wiki. Lakini Wenger ambaye pia hakufurahishwa na mchezo wa nguvu waliokuwa wakicheza Everton alisikitishwa na bao hilo kuruhusiwa baada ya kuonekana kuwa Romelo Lukaku alikuwa amezidi wakati akitengeneza nafasi ya kufunga bao hilo. Mbali na Lukaku kuzidi Wenger anaamini kuwa nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji pia alicheza faulo kwa beki wake Laurent Koscielny.

VURUGU BRAZIL, HELIKOPTA YATUA UWANJANI KUOKOA MAJERUHI.

MICHUANO ya Kombe la Dunia 2014 itakayofanyika nchini Brazil imeingia doa baada ya mashabiki watatu kuumizwa vibaya katika vurugu zilizotokea katika mchezo wa ligi ya nchi hiyo. Polisi wamedai kuwa mashabiki wa timu za Atletico Paraense na Vasco da Gama walikuwa wakipigana huku wakikimbia katika majukwaa katika Uwanja wa Catarina mara baada ya Atletico kufunga bao la kuongoza dakika ya 17 ya mchezo. 
Helikopta ya polisi ililazimika kutua uwanjani ili kumaliza vurugu hizo na kusaidia majeruhi kuwapeleka hospitali. Mchezo huo ulisimamishwa kwa saa moja kabla ya kuanza tena.

RATIBA YA KOMBE LA FA HADHARANI.

KLABU ya Arsenal imepangwa kucheza na wapinzani wao kutoka London ya Kaskazini, Tottenham Hotspurs katika mzunguko wa tatu wa michuano ya Kombe la FA. Kwa upande mwingine Manchester City wao watasafiri kuifuata Blackburn Rovers, Chelsea watakuwa ugenini kukwaana na Derby County wakati Manchester United wao watakuwa wenyeji wa Swansea. Mabingwa watetezi wa kombe hilo Wigan Athletic wataanza kampeni zao kwa kuikaribisha Milton Keynes Dons huku Liverpool wakimenyana wababe wao waliowafunga mabao 3-2 msimu uliopita timu ya Oldham au Mansfield. Mechi zingine za mzunguko huo zitakuwa kati ya West Bromwich dhidi ya Crystal Palace, Newcastle United dhidi Cardiff City na Norwich dhidi ya Fulham.