LONDON, England
MARA baada ya
Kocha Sir Alex Ferguson wa Manchester United kutangaza kuwa atastaafu
kufundisha soka, majina mengi ya makocha watakaochukua nafasi yake
yalitajwa. Jose Mourinho ambaye kipindi hicho alikuwa akiinoa Real
Madrid, alikuwa mmoja wa waliotajwa kwa wingi.
Bahati haikuwa
yake, Kocha David Moyes aliyekuwa Everton akapata nafasi hiyo, wengi
hawakutegemea, lakini inavyoonekana Mourinho aliumia, kwani inaaminika
ana mapenzi na Man United na bado anatamani kuifundisha timu hiyo licha
ya kuwa sasa ni bosi wa Chelsea.
Kutokana
na mwenendo mbaya wa United kipindi hiki, baadhi ya wachambuzi wa soka
wanaamini kuna uwezekano mkubwa wa kocha huyo kukubali kuifundisha
United hata leo hii endapo itatokea United imemtimua Moyes, kisha yeye
akahitajika kutua klabuni hapo.
Zifuatazo ni sababu chache
zinazoonyesha kocha huyo raia wa Ureno ana mapenzi na timu hiyo maarufu
kwa jina la Mashetani Wekundu licha ya kuwa anaiongoza vema Chelsea:
Kuonyesha heshima anapokutana nayo
Achana
na ile mara ya kwanza alipokuwa Porto, tangu Mourinho alipoondoka
England mara ya kwanza, amekuwa akiizungumza vizuri United na kuonyesha
heshima kubwa kwa Ferguson tofauti na makocha wengine.
Wakati
alipokuwa Madrid, siku timu yake ilipocheza dhidi ya United, Mourinho
alionekana kuwa mwenye nidhamu kubwa tofauti na awapo uwanjani wakati
timu yake ikicheza dhidi ya timu nyingine.
Hata mara baada ya mechi hiyo ambayo Madrid ilishinda, alisema: "Timu bora imepoteza mchezo.”
Kumtetea Alex Ferguson
Wakati
Ferguson alipomweka benchi straika wake tegemeo, Wayne Rooney, katika
Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, Mourinho alisema: "Sir Alex
ameshinda kwa kufanya maamuzi mengi magumu, kila anachofanya yupo sawa
na haihitaji maswali, ni kocha aliyetengeneza historia."
Kuitetea United ilipoyumba
Mwanzoni
mwa msimu huu, United ilikuwa ikiyumba kama ilivyo sasa, haikupata
matokeo mazuri, lakini Mourinho alipoulizwa alisema: “United ni United,
inaweza kufanya lolote na muda wowote.”
United bado ni timu kubwa
Mourinho
yupo Chelsea, ni timu kubwa lakini kwa sifa na rekodi za ubora bado
haijafikia kuwa daraja moja sawa na AC Milan, Barcelona, Liverpool, Real
Madrid, Juventus na Inter Milan, hivyo nafasi hiyo ni kubwa.
Heshima kila anapocheza dhidi ya United
Mara
kadhaa imewashangaza wengi kuwa Mourinho anapocheza dhidi ya timu kubwa
nyingine ni jambo la kawaida kukwaruzana na wapinzani, iwe wachezaji au
makocha, lakini anapofika Old Trafford huwa anaonyesha heshima na kuwa
mstaarabu.
Hana maneno ya ‘shombo’ akikutana na Mashetani hao,
lakini mara nyingi amekwaruzana na mabosi wa timu nyingine kama vile
Manchester City na Arsenal.
Kujulishwa na Ferguson kinachoendelea
Hivi
karibuni Mourinho alisema mara baada ya United kufanya maamuzi ya
kumchukua Moyes, alipata taarifa hizo mapema kutoka kwa Ferguson
mwenyewe, wengi wanajiuliza kwa nini kocha huyo mkongwe alienda
kumjulisha! Wanaamini kuna ukaribu zaidi ya urafiki juu ya taarifa hizo.
Katika
kura za maoni zilizopigwa kwenye mitandao barani Ulaya zinaonyesha kuwa
mashabiki wengi wa United wamekubali hoja kuwa United ingemchagua
Mourinho kuliko Moyes.
Kura hizo zipo hizi
Wanaomtaka Mourinho 80.9%
Wasiomtaka Mourinho 19.1%
Jumla ya kura: 8,114
Wewe
shabiki wa Tanzania unadhani Mourinho alikuwa ni mtu sahihi kuinoa
United? Tuma maoni katika namba 0719 137090. Maoni yako yatachapishwa
Ijumaa ijayo katika gazeti hili.
No comments:
Post a Comment