EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Wednesday, February 19, 2014

MWENYEKITI BUNGE LA KATIBA ..SITA NA CHENGE VITANI

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Kampeni za kuusaka uenyekiti wa kudumu wa Bunge Maalumu la Katiba zimeanza ndani na nje ya Bunge chini kwa chini.

Habari kutoka mjini hapa, zinaeleza kuwa kampeni hizo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya vigogo wanaotajwa kupigana vikumbo kupata nafasi hiyo.

Vigogo hao wamekuwa wakionekana wakiwazungukia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwafuata mmoja baada ya mwingine wakijaribu kutumia kila aina ya ushawishi kuwaomba wawaunge mkono katika harakati zao kuisaka nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo, kampeni hizo zilianza kufanywa na vigogo hao muda mfupi tu baada ya wajumbe wa Bunge hilo kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge juzi, ikiwa ni siku ya kwanza kwa Bunge hilo kuanza rasmi shughuli zake.

Mmoja wa vigogo hao alishuhudiwa na NIPASHE akihaha ovyo karibu ukumbi mzima wa Bunge akiwafuata wajumbe mbalimbali katika viti walivyoketi na kuanza kuteta na kila mmoja kwa wakati wake.

Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walithibitisha kwa nyakati tofauti kufuatwa na kigogo huyo na kuwaomba wamuunge mkono iwapo jina lake litapitishwa kuwania nafasi hiyo.

Habari hizo zinaeleza kuwa kigogo huyo hakuishia tu kuendesha kampeni zake ndani ya ukumbi wa Bunge.

Bali alishuhudiwa pia akihaha kuwashawishi wajumbe nje ya ukumbi wa Bunge. Vigogo, ambao wamekuwa wakitajwa kupigana vikumbo kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.

Chenge anatajwa kuungwa mkono na wabunge wengi wa CCM) wakati Sitta anatajwa kuungwa mkono na kundi la wajumbe, baadhi wakiwa wa CCM na wengi zaidi kutoka kundi la wabunge wa upinzani.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment