WATU mbalimbali na viongozi wa umma waliofaidika na fedha za akaunti
ya Tegeta Escrow ya Kampuni ya kufua umeme ya IPTL, wametakiwa kurejesha
fedha hizo, kufilisiwa mali zao na kushitakiwa mahakamani.
Aidha, mmiliki wa Kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi ameamriwa
kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa ya utakatishaji fedha
haramu, ukwepaji wa kodi na wizi.
Pia kwa kutumia sheria za nchi, kuhakikisha Sethi anarejesha fedha
zote alizochota Benki Kuu ya Tanzania, na kwamba kwa suala la
utakatishaji wa fedha haramu, mamlaka ziwasiliane na nchi nyingine
kuhakikisha mali za Sethi zinakamatwa na kufidia fedha hizo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imependekeza
hayo jana wakati ilipowasilisha bungeni mapendekezo yake kutokana na
matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki
Kuu ya Tanzania (BoT).
Akisoma mapendekezo maoni na mapendekezo ya Kamati baada ya
Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe kusoma sehemu ya uchambuzi wa sakata hilo,
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema Kamati inazitaka
mamlaka za uchunguzi kuhakikisha kuwa fedha hizo zinarudi Benki Kuu hata
kama ikibidi kufilisi mali za watu wote waliofaidika na fedha hizo
thamani ya fedha walizopewa na James Rugemalira, mmoja wa wanahisa wa
IPTL kupitia kampuni yake ya VIP Engineering.
“Kwa mujibu wa taarifa ya CAG na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru, fedha hizo pia ziligawiwa kwa watu mbalimbali binafsi. Kamati
haina tatizo na watu wawili kuuziana makampuni yao kwa thamani wajuazo
wenyewe, au jinsi ya kuzitumia fedha zao, ama kuwachagulia watu wa
kuwagawia, lakini Kamati imejidhihirishia kuwa sehemu iliyotumika
kulipia manunuzi hayo ni fedha ambayo sehemu yake ni ya umma iliyochotwa
bila huruma wala aibu, kutoka Benki Kuu,” alisema Filikunjombe.
Kamati hiyo ilisema Rugemalira aliuza hisa zake za VIP kwa Sethi
kutoka katika fedha za Tegeta Escrow, na kuthibitisha kuwa fedha hizo
zililipwa katika Benki ya Mkombozi Commercial Bank ambako ziligawawiwa
watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa umma, wanasiasa, watendaji wa
mashirika ya umma, watumishi wa umma, majaji na viongozi wa dini.
Zitto katika taarifa yake aliwataja viongozi wa kisiasa ambao
waliingiziwa fedha zao katika akaunti binafs ni Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa zamani na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Sh bilioni 1.6, Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuika, Sh
bilioni 1.6, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja,
Daniel Yona waziri mwingine wa zamani wa wizara hiyo na mbunge mstaafu
Paul Kimiti kila mmoja alipewa Sh. milioni 40.4 huku Dk Enos Bukuku
aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Tanesco aligawiwa Sh. milioni 101.7.
Kwa majaji, aliwataja Profesa Eudes Ruhangisa na Jaji J. Mujulizi
ambao mmoja alilipwa Sh milioni 404 na miwingine Sh milioni 40.4. Kwa
upande wa watumishi wa umma ni Philip Saliboko aliyekuwa RITA na
Emmanuel Ole Naiko aliyekuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kila mmmoja
alipata Sh milioni 40.4 na Lucy Apollo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ni
Sh milioni 80.8.
Kwa upande wa madhehebu ya dini, Zitto aliwataja Askofu Method
Kilaini million 80.8 Askofu Eusebius Nzigilwa Sh milioni 40.4 na
Mchungaji Alphonce Ye Simon alipata Sh milioni 40.4.
Zitto alisema baadhi ya watu hao walienda kugawana fedha benki tajwa
wakiwa na mifuko ya Rambo, sandarusi, maboksi, magunia na lumbesa.
Benki ya Mkombozi inamilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania. Kuhusu
watu hao, Filikunjombe alisema baadhi ya waliofaidika na fedha hizo ni
viongozi wa umma ambao wanapaswa kuzingatia Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma inayowataka kutoa taaria ya zawadi mbalimbali
wanazopokea au malipo wanayolipwa.
“Vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi kutambua kama walifuata
matakwa ya sheria na hatua mahsusi zichukuliwe ikiwemo kuvuliwa nyadhifa
zao zote za kuchaguliwa na/au kuteuliwa, kufilisiwa mali zao na
kushitakiwa mahakamani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Ibara ya 132 (1) – (6),” alisema.
Pia fedha zilizolipwa kwa PAP ambayo si mmiliki halali wa IPTL kwa
maana hiyo fedha hizo zilitolewa kwa watu hao kama rushwa na kutakatisha
fedha hizo haramu.
Kamati ilipendekeza kwamba akaunti zote zilizohusika na miamala
haframu ya akaunti ya Tegeta Escrow, akaunti zao zifungwe (freeze) na
wenye akaunti hizo walazimishwe kuzirejesha fedha hizo kwa mujibu wa
sheria ya Anti Money Laundering pamoja na mali zao kufilisiwa.
Aidha, Kamati imetaka kuvunjwa mara moja kwa Bodi ya Tanesco na
Takukuru iwafungulie mashtaka ta matumizi mabaya ya ofisi wajumbe wote
waliohusika kupitisha maamuzi hayo ya kifisadi ili iwe fundisho kwa
wajumbe wengine wa Bodi za mashirika ya umma kwamba watahukumiwa kwa
maamuzi mabovu wanayoyafanya.
SOURCE>>>HABARI LEO
No comments:
Post a Comment