Dar es Salaam. Siku chache
baada ya Rais Jakaya Kikwete kupokea taarifa kutoka kwa Mdhibiti na
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, utata wa kisheria
umegubika suala hilo kutokana na ukweli kuwa ibara ya 143 (4) ya Katiba
inataka Rais aiwasilishe bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema jana kuwa suala hilo lina madhara
katika utendaji wa Serikali.
“Kuna madhara makubwa katika mzunguko wa
uwajibikaji, kwani ni rahisi Serikali kuichezea taarifa ya CAG kabla
haijawa ya umma. CAG anakagua fedha za Serikali kwa niaba ya wananchi
kupitia Bunge. Hivyo ni lazima Bunge la Katiba lipishe Bunge la Muungano
ili kupokea taarifa ya CAG,” alisema Zitto.
Aliongeza: “Tangu uhuru, taarifa ya CAG
inawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Aprili kila mwaka. Kwa hali ya
sasa, Rais atakaa na taarifa hiyo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri
Bunge kukutana.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema siku hizo saba ni baada ya Bunge kuanza.
“Hakuna utata wowote hapo, ukisoma vizuri kifungu
hicho kinasema, Rais atamuagiza waziri anayehusika kupeleka taarifa hiyo
bungeni siku saba baada ya Bunge kuanza, siyo siku aliyokabidhiwa. Kitu
muhimu hapo ni pale kikao cha Bunge kinapoanza bila kujali kinaanza
lini,” alisema Balozi Sefue.
“Katika hali ya kawaida, Bunge la Bajeti lilipaswa
kuanza Aprili 8. Bunge la Katiba linahitaji pesa kutoka kwenye bajeti.
Sioni namna Bunge la Katiba kuendelea kwa sasa. Itabidi liahirishwe
mpaka Agosti,” alisema.
Suala la kuahirisha vikao vya Bunge la Katiba
kupisha Bunge la Bajeti lilielezwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
aliyesema atamshauri Rais Kikwete kuangalia uwezekano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila
akizungumzia uwezekano huo, alisema Bunge hilo litasubiri ratiba ya
shughuli za Bunge la Katiba.
Dk Kashilila alisema Kamati ya Uongozi wa Bunge la Katiba inatarajiwa kutoa ratiba ya shughuli zake kuelekea Bunge la Bajeti.
“Inapofika Juni, Serikali inatakiwa kuidhinishiwa
fedha kwa ajili ya matumizi yake, kwa hiyo mpango uliopo ni kuhakikisha
kabla ya Juni 30, Bunge la Bajeti liwe limeanza kazi zake,” alisema.
>>>MWANANCHI
>>>MWANANCHI
No comments:
Post a Comment