JINAMIZI la wachezaji wa Yanga kukosa penalti kisha
kuandamwa limeonekana kuendelea ambapo sasa makubwa yamemkuta
mshambuliaji wa timu hiyo, Hamis Kiiza baada ya kukosa penalti katika
mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, juzi.
Kiiza, raia wa Uganda, alikosa penalti hiyo katika dakika ya 71
ambapo matokeo ya mwisho ya mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar ni sare ya 1-1, hivyo Azam kuendelea kubaki kileleni
ikiwa na pointi 44, huku Yanga ikishika nafasi ya pili kwa pointi 40.
Mara baada ya kipenga cha mwisho cha mchezo huo, mashabiki wengi wa
Yanga walionekana kuchukizwa na kitendo cha timu yao kukosa ushindi,
lakini zaidi ikiwa ni baada ya Kiiza kukosa penalti hiyo, ambapo
walimvaa nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kuanza kumlaumu kwa
nini alikubali Kiiza apige penalti wakati wanaamini Cannavaro ni mzuri
kwenye mikwaju hiyo.
Kabla ya kutoka uwanjani hapo, wachezaji wa Yanga walijifungia na
kuanza kukosoana kutokana na kile kilichotokea kwenye mchezo huo ambacho
kimesababisha Yanga kuwa na kazi ngumu ya kutetea ubingwa wake.
Penalti hiyo iliyotokana na beki wa Azam, Said Morad, kuunawa mpira
kwenye eneo la hatari, ilipanguliwa kiufundi na kipa chipukizi Aishi
Manula.
Mara baada ya nusu saa kujifungia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo
uwanjani hapo, tangu mchezo ulipomalizika, walitoka huku wakionyesha
kuwa na hasira na kutoa lugha kali.
Alipotoka Cannavaro mashabiki waliokuwepo eneo la karibu na lango la
kutokea, wakamvaa na sehemu ya malalamiko yao yalikuwa hivi:
“Wewe ndiye mwenye timu yako, unaijua Yanga kitambo sana, siyo yeye
(Kiiza), timu ikiharibika atarudi kwao Uganda kisha sisi ndiyo
tutakaopata aibu hapa.
“Kwa nini hukupiga wewe ile penalti, sisi tuliona wewe unataka kupiga
yeye amekuja kuchukua mpira na kuupiga, jambo hilo siyo zuri kabisa
wala hatumfagilii, sisi tuna uchungu na timu hii kwani tunatoa pesa
zetu.”
Cannavaro alikuwa akiwajibu mashabiki hao kwa sauti ya chini ambayo
haikusikika kwa urahisi alichokuwa akikizungumza, alipoona umati
unaongezeka, akaondoka na kuingia kwenye basi.
Kiiza alipotoka vyumbani humo, alionekana ni mwenye huzuni, mashabiki
walianza kumtupia lawama, hakujibu kitu zaidi ya kuinama na kuanza
kulia huku akielekea kwenye basi la wachezaji.
Akiizungumzia penalti
hiyo, Aishi alisema ilikuwa ni ya kawaida: “Unajua sikuihofia kabisa
ile penalti, kwani ilikuwa ni ya kawaida sana kwangu, nimekuwa nikizoea
kudaka penalti tangu nilipokuwa katika timu B kwenye Michuano ya Uhai
Cup.”
>>>grobal publishers
No comments:
Post a Comment