Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipowasili
mkoani Dodoma jana. Wengine ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Bilal na
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana. Picha ya PMO.
Dodoma. Rais Jakaya Kikwete, jana aliwasili
mjini Dodoma katika kipindi ambacho Bunge Maalumu la Katiba liko
njiapanda baada ya wajumbe kushindwa kuafikiana kama upigaji wa kura uwe
wa siri au wa wazi.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye wajumbe wengi
katika Bunge hilo kimeweka msimamo wa kitaasisi kutaka kura ya wazi
ilihali vyama vya upinzani na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la wajumbe
201 walioteuliwa na Rais wakitaka kura ya siri.
Pia baadhi ya wajumbe wanaotokana na CCM wakiwamo
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi Zanzibar nao wameshikilia msimamo wa kutaka kura ya
siri.
Ingawa taarifa kutoka CCM zilidokeza kuwa ujio wa
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ni mahususi kwa
ajili ya kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC),
suala la kura linaweza kugusiwa.
Taarifa hizo zinadai agenda kuu ya CCM hiyo ni
kupitisha jina la mgombea ubunge katika Jimbo la Chalinze mkoani Pwani
ambapo mjumbe wa NEC ambaye ni mtoto wake, Ridhiwan Kikwete aliongoza
kura za maoni kwa kuwashinda Imani Madega na Ramadhani Maneno.
Habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya
Mashauriano, zilieleza kuwa kamati hiyo imeshindwa kufikia mwafaka
kuhusu utaratibu gani utumike katika upigaji wa kura na mtu
anayetegemewa kukoa jahazi ni Rais Kikwete.
“Jana (juzi) walituambia kuwa kwa vile Rais
angewasili leo (jana) basi wanaomba muda wafanye mashauriano naye na
ikibidi waangalie uwezekano wa kuitisha mkutano wa ndani wa chama wa
dharura kujadili hili jambo,” alidokeza mjumbe mmoja.
Mjumbe huyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe,
alisema baada ya kukutana na Rais, wajumbe wa kamati hiyo ya mashauriano
wanaotokana na CCM watawasilisha mrejesho wa nini wamekubaliana kwenye
kikao ili leo, vifungu 37 na 38 ambavyo vimekwama viweze kuridhiwa.
>>>mwananchi
>>>mwananchi
No comments:
Post a Comment