HATIMAYE Rais Yoweri Museveni amesaini
Muswada wa Sheria inayoharamisha na kutoa adhabu kali kwa wanaojihusisha
na vitendo vya ushoga nchini na wanaowaficha. Msemaji wa Serikali,
amesema Rais alitaka kutetea “uhuru wa Uganda dhidi ya shinikizo la
mataifa ya Magharibi.”
Rais Barack Obama wa Marekani
alishahadharisha dhidi ya Muswada huo, akisema kuwasilishwa kwake
kunaashiria Taifa la Uganda linapiga hatua moja nyuma. Rais Museveni
awali alikubali kuweka pembeni Muswada huo, akisubiri ushauri wa
kisayansi kutoka Marekani.
Vitendo vya ushoga nchini hapa tayari ni
haramu. Desemba mwaka jana, mwanaharakati mtetezi wa haki za mashoga,
alielezea hofu yake juu ya sheria hiyo.
Sheria hiyo mpya inatoa adhabu kwa
wakosaji wa kwanza kufungwa miaka 14 jela na inaruhusu adhabu ya kifungo
cha maisha jela kwa vitendo vya “ushoga uliopindukia.”
Pia kwa mujibu wa sheria hiyo, ni kosa
la jinai kwa mtu ambaye hatafichua mashoga, halikadhalika ni kosa la
jinai “kutangaza” na hata “kutambua tu” uhusiano wa kishoga “kupitia au
kwa msaada wa chombo chochote cha serikali nchini au asasi yoyote isiyo
ya serikali ndani na nje ya nchi.”
Wasagaji nao kwa mara ya kwanza
wameguswa na sheria hii. Lakini wanaharakati wanaotetea haki za mashoga,
wamesema watapinga sheria hiyo mpya mahakamani.
Awali Muswada huo ulikuwa unapendekeza
adhabu ya kifo kwa vitendo vya ushoga, lakini baadaye ilibadilishwa
kutokana na kelele za kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP,
maofisa wa Serikali walipiga makofi baada ya Rais Museveni kusaini
Muswada huo mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu jijini hapa jana.
BBC inaripoti kwamba ni mara chache sana kwa Rais kusaini miswada
hadharani. Lakini Muswada huu ulikumbwa na utata mkubwa, hivyo
kusababisha wanahabari kuitwa kushuhudia ukisainiwa.
Mapema, Msemaji wa Serikali, Ofwono
Opondo aliiambia Reuters, kwamba Rais Museveni alitaka "kuthibitisha
uhuru wa Uganda licha ya uchokozi na shinikizo la Magharibi.” Mtetezi na
muasisi wa Muswada huo, Mbunge David Bahati, alisisitiza kuwa ushoga ni
“tabia ya kujifunza na inaweza kukomeshwa pia.
“Ushoga ni tabia mbaya, ambayo haipaswi
kuruhusiwa katika jamii yetu,” aliiambia BBC. Lakini mwanaharakati wa
haki za ushoga nchini alisema “ametishwa,” sana na sheria hiyo mpya.
“Sikwenda hata kazini leo (jana). Nimejifungia ndani. Na sijui ni nini
kitatokea sasa.
Nazungumza na wanaharakati wangu wote
kwa simu. Nako ni hivi hivi, wamejifungia majumbani mwao. Hawawezi
kutoka nje. Wamekaa wanaangalia kinachoendelea.” Kusainiwa kwa Muswada
huo kunaonesha mgeuko wa ghafla kutoka ahadi ya hivi karibuni ya kuuweka
kando ukisubiriwa ushauri kutoka Marekani. Katika kauli yake, Museveni
alisema:
“Naisihi Serikali ya Marekani kutusaidia
kwa kushirikiana na wanasayansi wetu, kutafiti ili kujua kama, hakika,
kuna watu wanazaliwa wakiwa mashoga. Hilo litakapothibitishwa, tunaweza
kupitia upya sheria hii.”
Obama akasirika Rais Obama aliielezea
hatua hiyo kama ni “zaidi ya tusi, na hatari kwa, jamii ya mashoga wa
Uganda. Itakuwa ni kupiga hatua moja nyuma kwa Waganda wote.”
Alionya kwamba hatua hiyo itasababisha
“ugumu” katika uhusiano wa Marekani na Uganda, ambayo inapokea msaada wa
dola milioni 400 kwa mwaka kutoka Taifa hilo kubwa.
Nako Afrika Kusini, Askofu Mkuu wa
zamani Desmond Tutu alisema amekatishwa tamaa na Rais Museveni kutokana
na kubadili msimamo wake.
>>>Habari leo
No comments:
Post a Comment