CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeamua kuwasha moto nchi nzima kwa
wiki mbili mfululizo kuanzia leo, ukiwa ni mkakati wa kujiimarisha na
kujadiliana na wananchi kuhusu masuala nyeti ya kitaifa.
Katika
kutekeleza azima hiyo, chama hicho kimejigawa katika makundi makuu
matatu, na vikosi vidogo sita, yatakayowashirikisha viongozi wakuu wa
chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda za chama.
Operesheni
hiyo imepewa jina la ‘M4C Pamoja Daima’ ikiwa na lengo la kuwafikisha
viongozi hao katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kupeleka ujumbe kwa
umma kupitia ajenda tisa (9) zilizopendekezwa na Kamati Kuu katika kikao
chake kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.

Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr Wilbroad Slaa akiwasili Songea.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu ya chama hicho,
Kinondoni, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema
ni operesheni maalumu yenye lengo la kuimarisha chama na kuwapa wananchi
fursa ya kujadili masuala muhimu yanayogubika taifa mwanzoni mwa mwaka
2014.
Ajenda hizo
ni mchakato wa katiba mpya katika hatua ya Bunge la Katiba na kura ya
maoni; daftari la kudumu la wapiga kura; uchaguzi wa madiwani katika
kata 27; ujenzi wa chama ngazi za chini; uchaguzi ndani ya chama;
uchaguzi serikali za mitaa na kuandaa umma kwa uchaguzi mkuu 2015.
Vile vile,
viongozi hao watajadili kero zinazowakabili wananchi; na watafika katika
Jimbo la Kalenga kuhani msiba, na kuwapa pole wananchi kwa kufiwa na
mbunge wao, William Mgimwa aliyekuwa pia Waziri wa Fedha.
Mbowe
alisema operesheni hiyo imegawanyika katika makundi makuu matatu.
Makundi hayo yatagawanyika katika vikosi sita; vitatu vya angani kwa
kutumia helikopta na vitatu vya ardhini kwa kutumia magari.
Mbowe
alisema chama hicho kimegubikwa na matukio makubwa ya kisiasa ukiwamo
uchaguzi wa ndani na ule wa serikali za mitaa, na kwamba wanahitaji
kujipanga ipasavyo kuweza kukabiliana na hali hiyo.
“Hatufanyi
kampeni bali huu ni mwendelezo wa maandalizi ya uchaguzi mbalimbali.
Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa 2015 pale tulipomaliza
uchaguzi mkuu uliopita, na sasa tunachofanya ni kuongeza nguvu na
umakini zaidi katika muda huu,” alisema Mbowe.
Misafara ya
helikopta na magari katika operesheni hiyo itaanzia katika mikoa ya
Tanga, Mwanza na Ruvuma. Katika kila eneo, viongozi hao watapita katika
kata zote zinazotarajiwa kufanya uchaguzi wa marudio kwa ajili ya
madiwani ili kuwaongezea nguvu wagombea wa CHADEMA.
Vile vile,
watapita katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mikakati kadhaa ya
utekelezaji wa maagizo ya serikali kama Operesheni Kimbunga na
Operesheni Tokomeza Ujangili.
Baadhi ya
makada wa CHADEMA waliozungumzia operesheni hiyo, walisema inalenga
kuelekeza nguvu ya chama katika masuala ya msingi na kuimarisha umoja
miongoni mwa wanachama.
Kwa
msisitizo wa pekee, Mbowe alionya serikali isifanye mzaha na daftari la
kudumu la wapiga kura, akisema mzaha wowote wa aina hiyo ni kuchezea
amani ya nchi.
Alisema
CHADEMA imeshajua mbinu za serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kukwamisha mchakato wa katiba mpya, na kutoandikisha wapiga kura katika
daftari la kudumu, na kwamba kama CCM wanadhani watazuia katiba mpya
kupatikana kistaarabu, CHADEMA itatumia njia mbadala kuhakikisha
wananchi wanapata katiba wanayotaka.
“Hakuna
kurudi nyuma kwenye suala la katiba mpya. Wakichezacheza na mchakato wa
katiba mpya, tutaitafuta kwa utaratibu mwingine,” alisisitiza.
Alisema
watatumia ziara hii kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha
katika daftari hilo, na kuitaka serikali itumie muda huu kuandikisha
wananchi wote wenye sifa ambao hawajajiandikisha kupiga kura kwa sababu
mbalimbali.
Miongoni mwa
kazi watakayoifanya katika ziara hizo ni kuelimisha wananchi na
kuwahamasisha kuchukua hatua iwapo serikali itagoma kuboresha daftari
hilo.
Hadi sasa
inakisiwa kuwa wananchi wapatao milioni nne, hasa vijana,
hawajaandikishwa katika daftari la kupiga kura kwa visingizio kadhaa vya
Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kisingizio kikubwa kinachotolewa ni ukosefu
wa fedha za kufanyia kazi hiyo.
Mbowe
alisema watahamasisha Watanzania wasishiriki mchakato wa kura ya maoni
iwapo serikali itagoma kuboresha daftari hilo, lakini haina maana ya
kususa, bali kutafuta njia mbadala ili kunusuru taifa lisiingie katika
machafuko.
Alisema kama
Serikali ya CCM inataka amani iendelee kuwepo wasifanye mzaha katika
suala la katiba kwani si la CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi bali ni
mustakabali wa Watanzania.
Mbowe
alisema kuwa sheria inaelekeza daftari la kudumu la wapiga kura
kufanyiwa maboresho kati ya uchaguzi na uchaguzi ili kuwapa nafasi watu
waliohama maeneo yao, waliopoteza vitambulisho na waliotimiza sifa ya
kujiandikisha.
Alisema kuwa kuendelea kuwaacha nje watu hao ni kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
“Kama katiba
haitapita kwa sababu ya kushindwa kuboreshwa kwa daftari la kudumu,
wasidhani tutarudi katika katiba ya zamani. Hiyo ni ndoto ya CCM.
“Nawaambia waache, na kama serikali inataka amani wasifanye mzaha katika suala la katiba,” alisema.
Taswira za Uzinduzi wa Operesheni Pamoja Daima Mkoani Ruvuma
Dr Slaa akiwahutubia wakazi wa Songea.
Dr Slaa akiwahutubia wakazi wa Mbinga
Dr Slaa akiwahutubia wakazi wa Namtumbo.
Mbunge wa Iringa Mjini Mh Peter Msigwa akiwahutubia wakazi wa Mbinga.
Msigwa akiwahutubia wakazi wa Songea.
Taswira za Uzinduzi wa Operesheni Pamoja Daima Mjini Uyui
Mbunge wa Ubungo Mh John Mnyika akiwahutubia wakazi wa Uyui, Tabora katika uzinduzi wa Operesheni Pamoja Daima
Wakazi wa Uyui waliohudhuria katika uzinduzi wa Operesheni Pamoja Daima





No comments:
Post a Comment