Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kuna haja ya taasisi za mafunzo ya uongozi za China na Tanzania kuandaa kozi zenye kuwafaa makundi fulani ya viongozi ambazo zitasaidia kubadili mwelekeo wao na utendaji kazi hasa katika masuala yanayohusu sekta binafsi.
![]() |
waziri mkuu wa Tanzania-MH:Mizengo Pinda |
Alisema Tanzania imefanya maamuzi ya kutumia ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP) kama njia ya kukuza na kuendeleza miundombinu, kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na ujenzi wa viwanda.
“Ni muhimu taasisi zetu hizi mbili zikatambua jambo hili na kuchangia kwa juhudi zote ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa,” alisema.
Alisema kozi kama hizo zinapaswa kuwalenga watumishi kutoka taasisi za serikali pamoja na sekta binafsi na akazitaka taasisi hizo kuhakikisha zinasaidia kuwepo kwa ufanisi wa hali ya juu kwenye ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma.
“Muwasaidie watu hawa waweze kutambua ni wakati gani ushirikiano wa aina hii unakuwa wa manufaa zaidi kwa wahusika, ni wakati gani wahusika wanafaidika na PPP, je wanakabiliwa na changamoto zipi, na wanafanyaje ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza,” aliongeza.
Alisema jambo lililo wazi kuwa ushirikiano baina ya wajasiriamali wa Kichina na wa Kitanzania utasaidia kuongeza fursa za kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na kuendeleza miundombinu.
“Natambua kwamba kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa kutoka China ambao wako nchini Tanzania, hawa wanachangia maendeleo ya kiuchumi Tanzania kwa kuingiza teknolojia mpya na kutoa fursa za ajira,” aliongeza.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tatu ya ziara ya siku tisa ya kikazi kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alitembelea kiwanda cha aluminium cha China (CHINALCO) na kiwanda cha kutengeneza zana za kijeshi ambako alionyeshwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda hivyo.
No comments:
Post a Comment