Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Habari zinaeleza kuwa katika mkakati huo, chama hicho kinakusudia kuweka utaratibu wa kupata mgombea wake mwaka huu badala ya mwakani.
Vyanzo vyetu ndani ya CCM vimeeleza kuwa kupitia mkakati huo, chama hicho tawala kinataka kumpata mpeperusha bendera yake kabla ya kumalizika mwaka huu.
Hadi sasa hazijafahamika sababu zinazoshinikiza chama hicho kuingia katika jaribio la kubadilisha utaratibu wa kupata mgombea wake, ambaye kwa kawaida hupitishwa kabla ya Julai ya mwaka husika wa uchaguzi.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya chama hicho zinadai kuwa, msukumo huo unabebwa na mbinu ya kuwaweka kando makada sita waliopewa onyo kali na kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia Februari mwaka huu.
Kama utaratibu huo utatumika kumpata mgombea urais wa CCM ni dhahiri makada hao, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia January Makamba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja hawataruhusiwa kugombea katika chaguzi za kuwashindanisha makada wa chama hicho ili baadaye kupata mgombea mmoja mwaka 1995 na mwaka 2005.
Katika uchaguzi wa mwaka 1995 Benjamin Mkapa alitangazwa kuwa mshindi Juni baada ya kuwashinda Jakaya Kikwete na Cleopa Msuya.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Jakaya Kikwete pia aliteuliwa Juni baada ya kuwashinda Dk. Salim Ahmed Salim na Profesa Mark Mwandosya.
Mmoja wa makada wa chama hicho, alisema kama ni kweli utaratibu huo utabadilishwa kutakuwapo na sababu maalum, lakini alisema kama zingekuwapo, chama kingepaswa kutoa taarifa kwa wanachama wake mapema.
Kada mwingine alisema kama kuna mkakati huo utakuwa na lengo la kuwazuia makada wake sita ambao wametuhumiwa kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.
Chama hicho juzi kilitangaza kuwapa onyo kali viongozi na makada wake sita waliobainika kuanza kufanya kampeni za chini kwa chini kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mwakani.
Mbali na kupewa onyo kali, makada hao pia wametakiwa kutojihusisha na kampeni au vitendo vyovyote vinavyoashiria kampeni na watakuwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja.
Aidha, CCM imewatangazia makada hao kuwa wakikiuka agizo hilo, watakuwa wamejiondolea sifa ya kushiriki mchakato wa kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama chao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imefikia hatua ya kuwaonya makada hao baada ya kuwabaini kuwa wameanza kufanya kampeni za kutaka wateuliwe na chama hicho kugombea nafasi za uongozi.
Nape alisema makada hao walihojiwa na kamati ya maadili na kwamba wote walibainika kuanza kampeni kinyume cha maadili na kanuni za chama hicho; hivyo kamati ilipendekeza kuwa wote waadhibiwe.
Nape aliongeza kuwa kazi ya kutoa adhabu ilikuwa ni ya kamati kuu ya CCM ambayo hatimaye ilikaa na kutekeleza wajibu wake wa kutoa adhabu na onyo dhidi yao.
Mwanachama mwingine wa chama hicho, alisema kuwa mkakati wa kutangaza mgombea urais unalenga kuwaengua makada hao sita kwa kuwa kama wamezuiwa kugombea uongozi ndani ya miezi 12 watakuwa wamekosa sifa kugombea urais ikiwa mgombea atatakiwa kupatikana Desemba.
Kwa mujibu wa adhabu hiyo, wagombea hao kama hawatapatikana na kosa lolote la kufanya kampeni kabla ya wakati, watakuwa huru kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama kuanzia Februari mwakani.
Membe akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhojiwa Jumapili iliyopita, miongoni mwa mambo aliyoyazungumza, alisema anapendekeza chama hicho kuanzisha utaratibu wa kumpata mgombea Desemba mwaka huu na kutaka kuandaliwa midahalo ili wananchi wawafahamu vizuri wagombea.
KAULI YA NAPE
Hata hivyo, NIPASHE lilipomuuliza Nape kuhusiana na madai ya kuwapo kwa makakati huo, alisema suala hilo halipo na kwamba halijazungumzwa ndani ya vikao vya chama.
“Labda itokee baadaye, lakini kwa sasa hakuna kitu kama hicho,” alisema Nape.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment