EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Saturday, September 6, 2014

Ndanda Fc wanakijiji wanaokuja kuliteka soka la bongo.



Kikosi cha timu ya Ndanda Fc, kipindi kipo kinashriki Ligi Daraja la Kwanza

Imeandaliwa na Mshamu Ngojwike
NI wanakijiji haswa! Walianza kama utani, kijiwe cha wazee wenye busara tu na ndio waanzilishi wa timu. Si wengine ni Ndanda Fc, ambao wameleta gumzo kubwa kila kona mitaa ya Mkoa wa Mtwara, ama kwa hakika wamewarudisha kwenye enzi za Bandari Fc.

Gumzo hilo si kwa mkoa wa Mtwara tu, hata wapenzi wa  kandanda la hapa bongo walifuatilia toka kupanda kwao Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Ndipo ikaanza minong'ono mingi huku wakihoji uwezo walio nao wakusakata kabumbu  vijana hawa wameutowa wapi? Pamoja na sapota kubwawanayoipata kutoka kwa mashabiki wa mikoa ya kusini mwa Tanzania ya  Lindi na Mtwara.

Mashabiki hawa walionyesha mbwenbwe haswa toka timu hiyo ikiwa ligi daraja la kwanza iwe kwenye uwanja wa nyumbani ama nje ya Mtwara walikuwa wanatoa nguvu kubwa ya kuisapoti.
Kwa wakifuata falsafa ambazo wakitumia mashabiki wa Mbeya City msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara,na muda ule wapo Ligi Daraja la Kwanza(FDL) nao.

Ndanda ilikuwa timu ya kwanza kufanikiwa kupanda daraja msimu huu,baada kufanikiwa kuongoza kwenye kundi A kwa pointi 28 ikiwa mbele kwa alama moja ya African Lyon iliyomaliza ligi daraja la kwanza(FDL) kwa alama 27.

Lilikuwa kundi ambalo lilitawaliwa timu za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zinatambua radha ya Ligi Kuu zikiwemo African Lyon,Tessema,Friends Rangers na Polisi Dar.

Mbali na Ndanda Fc, timu nyingine zilizopanda Ligi Kuu Mwaka huu ni pamoja na Stand United ya Shinyanga na Polisi Morogoro kwa kuchukua nafasi ya Rhino Rangers, JKT Oljoro na Ashanti United zilizoshuka daraja.

Zikiwa zimesalia siku chache ili msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2014/2015 uanze kunguruma kwenye viwanja tofauti hapa nchini, kila timu ipo katika maamdalizi ya kuanza msimu mpya wa Ligi kwa kuweka kambi mikoa  tofauti tofauti ya hapa nchini.

Wageni hao, waliweka kambi yao ya  siku 40 jijini Dar es Salaam huku wakichimbia kwenye Chuo Kikuu cha Ardhi wakijiwinda na Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Septemba 20 mwaka huu.
Mtandao huu ulitinga kwenye makao makuu ya klabu, kijijini kwao Ndanda Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara. Na kudaka  historia ya ndanda Fc na Mikakati yao kwenye Ligi mwaka huu, ambayo ilisimuliwa na mwenyekiti Ahamadi Omari Ally.
 wanamtwara kuchele ndani ya ligi daraja la kwanza



HISTORI YAO

 Mwenyekiti wa Ndanda Fc, Ahmadi Omari anasimulia kuwa  ilikuwa Machi 2011 yeye pamoja na Jofrey Lukanga 'Jb' walipokutana na  wakashaulina kunzisha timu maeneo ya Shule ya Msingi Ndanda, ili kuleta upinzani na timu ya sokoni boda boda Fc, huku ikifahamika kama Madukani Fc.
Ndipo mwezi huo huo waliianzisha timu ya Ndanda Fc,wakiwa na lengo la kukuza vipaji kwa  vijana wa kijiji cha Ndanda pamoja na kusini kwa ujumla.

Aprili 2011, waliona si busara kuwa na timu bila uongozi ndipo wakachagua benchi la viongozi ambao waliongoza kikosi hicho chini ya  mzee Ahmadi Omari kama Mwenyekiti,Jofrey Lukanga mlezi wa timu kutokana yeye alikuwa vizuri kiuchumi na John Mnunduma katibu.

Kwa muda huo kulikuwa na upinzani mkubwa katika kijiji, baina ya timu ya Boda boda Fc,Sokoni Fc,wao Ndanda Fc na timu ya Kiwanda cha maji ya Ndanda ambayo ikifadhiliwa na meneja wa kampuni Mohamedi Mamu kutokana na kandanda safi ambalo walikuwa wanaonyesha enzi hizo.

Lakini nyota ya Ndanda Fc ilianza kung’aa toka mwaka huo huo wa 2011 baada ya  kushiriki kombe la kugombea jezi na mipira miwili ambalo liliandaliwa na Chama cha Soka Wilaya ya Masasi na kuafanikiwa kuibuka mabingwa wa michuano hiyo.

Ndipo Mwishoni mwa mwaka huo, timu hiyo ilishiriki ligi daraja la nne, na walifanikiwa kupanda daraja hadi la tatu baada ya kuongoza kwa pointi kwenye mzunguko , ambapo anasema muda huu timu ilikuwa chini ya kocha Samsoni Mrope ambaye kwa sasa ni fundi gereji.

2012, walishiriki kwa mara ya kwanza ligi daraja la ngazi ya Wilaya ya Masasi.Pia, hapa walifanikiwa kupanda hadi ligi daraja la pili ngazi ya Mkoa wa Mtwara baada ya kuongoza kwa alama kwenye hatua ya mzunguko na kuwa mwakilishi wa Wilaya ya Masasi.

Anasema 2012 hiyo hiyo,walicheza ligi daraja la pili mwishoni mwa mwaka ili 2013 ipatikane timu ambayo itawakilisha Mkoa wa Mtwara kwenye ligi daraja la kwanza(FDL) ngazi ya taifa.Napo ilikuwa njia nyepesi kwao, maana walifanikiwa kupanda kwa mara ya kwanza kushiriki ligi daraja la kwanza.

Walianza kushiriki ligi daraja la kwanza 2013, ambapo hawakufanya vizuri walishika nafasi ya 3 kwenye kundi A, huku Ashanti United wakipanda msimu huo.

2014 ilikuwa mara yao ya pili kushiriki ligi daraja la kwanza na kufanikiwa kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kusota kwa kipindi hicho cha miaka miwili, huku zikizibwaga timu za mkoa wa Dar es Salaam.

CHIMBUKO LA JINA LA NDANDA FC:


Walitoa heshima ya mto wa Ndanda ambao kwa wakazi wa kijiji hicho huutumia kwa shughuri zao za kila siku pamoja na  kilimo kando kando yam to huo. Pia, Kampuni ya Maji ya Ndanda ‘Ndanda Springs Water’ hutumia maji ya mto huu na kuyatengeneza kwa kuyachuja na kuyasambaza, ndipo wakaona wautangaze mto huu kwa kutumia mpira na kuipa jina timu hii, jima la Ndanda Fc.

JINA UTANI

Kila timu za hapa nyumbani hazikosi kuwa na jina la utani, kwa upande wa timu ya Ndanda wao hufahamika kama ‘Walima Maji’. Baada ya timu hii kuanza kufadhiliwa na Kampuni ya Maji ya Ndanda spring Water chini ya mkurugenzi wa kiwanda Mohamedi Mamu pindi wakiwa Ligi Daraja la pili.
Muda huo maji yalikuwa yakipatikana kwa wingi katika michezo yao, pamoja ya sifa ya mto Ndanda ndipo wakawapachika jina la walima maji.

KAULI MBIU

Kama uliwahi kushuhudi michezo yao muda wakishriki Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita basi mashabiki wao, walikuwa wanastahili mpya  ya ushangiliaji ya kuiimba Ndandaa! Ndandaa! Kwa roho safi…! Na ndiyo wamehitumia kuwa kauli mbiu yao kuwa ‘kwa roho safi’.
Wakimaanisha kuwa ukiipenda timu yao basi utakuwa mtu wa furaha na uwe umeipenda toka kwenye moyoni.

MWENYEKITI WA TIMU

Klabu hii inaongozwa na mzee Ahmadi Omari Ally, ndiyo mwanzilishi wa timu,alianza kuongoza  toka 2011 hadi inaipanda ligi Kuu ikiwa chini ya uongozi wake.

KATIBU WA KLABU

Edmund Njoweka ndiyo katibu Mkuu wa klabu. Alipata nafasi hii baada ya timu kuibadirisha kutoka mikononi mwa wanachama hadi kuwa chini ya kurugenzi.

Ambapo ilibidi wagawane wajumbe sita kutoka Mtwara mjini na sita toka Ndanda kijijini, ndipo katibu huyu mkuu alipopta fursa ya kuongoza kuanzia mwaka huu.

NAHODHA
Baada ya kufanya usajili wa nguvu, wakaamua kumpa nahodha mzawa toka nyumbani kwa Masasi Paul Ngalema.

 KOCHA MKUU

Kocha Mkuu wa timu hii Denis Kitambi,alichaguliwa baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Amri Saidi ambaye aliibwaga ikiwa katika nafasi mbaya huku ikikabiliwa na michezo migumu na kufanikisha kuipandisha daraja. Ndipo uongozi wa timu hii wakaona ni bora waendelee naye.

UWANJA

Ndanda Fc watatumia Uwanja wa Nangwanda Sijaona zamani ukijulikana kama Umoja. Mwaka huu, Uwanja huu umefanyiwa ikarabati ili kuwa kwenye hadhi ya kutumika kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

MALENGO YAO
Anasema wamejipanga kuleta ushindani kwenye Ligi Kuu mwaka huu, na wasidhani kama wamekuja kupanda pantoni yaani kupanda na kushuka la hasha! Wamejidhatiti kuja kuonyesha maajabu ili kuwa miongoni mwa timu vigogo hapa nchini.


USAJILI

Sehemu kubwa ya kikosi chao kitaundwa na  vijana 14 ambao wameipandisha Klabu hiyo toka Ligi daraja la kwanza(FDL), huku wakifanya usjili wa wachezaji 13 ambao ni wazoefu wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika idadi ya wanandinga 27 waliowasajili.
 Wanaamini usajii wachezaji walio ingia nao ni makini hivyo waweza kumudu mikiki mikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

UDHAMINI


Miongoni mwa Klabu imepata bahati ya mtende mwaka huu, ni pamoja na timu ya Ndanda. Hii ni kutokan ni mara ya kwanza kushiriki ligi na wamepata wadhamini watatu nje na wadhamini wa Kuu wa Ligi Vodacom na Azam tv.

Ndanda Fc, wanamaji ya Ndanda Spring Water,Kampuni ya gesi ya BG Tanzania na Bin Slum ambao wameingia udhamini kwenye klabu hiyo.

Kujiweka Kibiashara
Amesema watauza vifaa mbali mbali ambavyo waliagiza toka China katika mechi zao za  Ligi Kuu Tanzania bara mwaka huu, lakini aliwataka wapenzi wandanda Fc  kutonunua vifaa feki zenye nembo ya timu ya Ndanda kwani hadi sasa haijaanza kusambaza vifaa vya aina yeyote nchini.

Vifaa hivi wameagiza kutokana na soko lao la biashara na mahitaji husika ya eneo lao la kanda ya kusini.Ambapo wameagiza jezi,kanga,kalenda na Stika vyema nembo ya timu ya Ndanda Fc.

Sapoti ya Mkoa
Chama Cha Soka Mkoa wa Mtwara(MTWAREFA)  kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ipo bega kwa bega kwa kuwatafutia wadhamini kama BG Tanzania ni nguvu ya Mkuu Mkoa wa Mtwara Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia.

Walitumia harambee ya kuwakutanisha viongozi mbali mbali kwenye kampeni ya Changia Ndanda Ishinde wakati ipo kwenye mchakato wa kutafuta nafasi nya kupanda ligi kuu msimu huu.

Jina la timu:Ndanda Fc
Jina la Utani:Walima maji
Ilianzishwa:2011
Mwenyekiti:Ahmadi Omari Ally
Katibu:Edmund Njoweka
Kocha Mkuu:Denis Kitambi
Nahodha:Paul Ngalema
Uwanja:Nangwanda Sijaona

No comments:

Post a Comment