NYOTA sita wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC wamekalia kuti kavu baada ya kupigiwa mstari mwekundu wa kutohitajika katika kikosi cha timu hiyo msimu ujao.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Azam
FC, kimewataja nyota waliopigiwa mstari huo kuwa ni Ibrahim Mwaipopo, ambaye
amekuwa majeruhi kwa muda mrefu, Jabir Aziz na Seif Karihe ambao watapelekwa
kwa mkopo moja ya klabu za Ligi Kuu.
Kilieleza uongozi wa Azam FC bado unatafakari Karihe
aende timu gani ambayo itamsaidia kuimarisha kiwango chake, kwa kuwa ni
miongoni mwa wachezaji ambao timu hiyo ina malengo naye ya muda mrefu.
Nyota wengine wanaotemwa ni Malika Ndeule, Kipre
Bolou, Ismail Kone na Lackson Kakolaki ambaye atapelekwa shule kusomea ukocha
kwa ajili ya kuandaliwa kuifundisha timu ya vijana ya klabu hiyo.
Tayari Azam ipo katika mchakato wa kuvunja mkataba
na Bolou na Kone ambao ni raia wa Ivory Coast yakiwa ni mapendekezo ya kocha
wao, Joseph Omog baada ya kuangalia upungufu wa kikosi chake na uhitaji wa
nyota wapya kujiwinda na michuano ya kimataifa na Ligi Kuu.
“Sasa tunatakiwa kujipanga kimataifa kwa kufanyia
kazi dosari zilizojitokeza kwa kuwapunguza na kuongeza wachezaji watakaosaidia
timu kwa ajili ya safari ya kutetea ubingwa wetu na ushiriki wa michuano ya
Ligi ya Mabingwa Barani Afrika,” alisema.
Baadhi ya wachezaji waliomaliza mikataba yao lakini
bado wana nafasi katika kikosi cha timu hiyo baada ya kumkuna Omog kwa kiwango
chao ni mshambuliaji, Gaudence Mwaikimba na beki Said Morad ambaye Yanga
inamuwania kwa udi na uvumba.
SWACOTZ FORUM lilipomtafuta Katibu Mkuu wa timu hiyo, Nassor
Idrissa alisema, ni mapema kuzungumzia wachezaji wanaoachwa lakini itakapofika
muda wake mambo yote yatawekwa hadharani.
No comments:
Post a Comment