EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Monday, April 14, 2014

Upigaji kura kupitisha sura mbili zinazohusu Muungano katika Bunge la Katiba umesogezwa mbele hadi Agosti litakapoitishwa tena, Mwananchi limebaini.

Dodoma.
Vyanzo mbalimbali vimelidokeza gazeti hili jana kuwa upigaji kura hautafanyika sasa badala yake wajumbe wa Bunge wataendelea kuchangia hoja hadi Aprili 28, mwaka huu wakati Bunge hilo litakapoahirishwa baada ya kukamilisha siku 70 za awali.
Awali, upigaji huo wa kura ambao umewagawa wajumbe katika makundi mawili; moja likitaka serikali tatu na jingine likitaka serikali mbili, ulitarajiwa kufanyika Ijumaa wiki hii ili kuhitimisha mvutano wa muda mrefu baina ya pande zinazopingana.
Chanzo chetu ndani ya Kamati ya Uongozi, kilidokeza jana kuwa hata baada ya Bunge hilo kurejea Agosti 5, mwaka huu, ikielezwa kuwa lengo ni kutoa fursa ya kuendelea kushawishi uungwaji mkono ili kupata theluthi mbili ya kura inayohitajika.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alithibitisha kuahirishwa kwa upigaji wa kura huo, lakini akasema hiyo imetokana na wingi wa wajumbe wanaotaka kuchangia na si kitu kingine.
“Ni kweli wajumbe hawatapiga kura kwa sura mbili walizowasilisha hadi jana na lengo ni kuwapa nafasi wajumbe wengi zaidi kuchangia katika jambo hili zito,” alisema Sitta.

Alisema hadi jana mchana alikuwa amepokea majina ya wachangiaji zaidi ya 400 ambao wasingeweza kuchangia kwa siku tatu kama kanuni zinavyoelekeza.
Hata hivyo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi zaidi juu ya jambo hilo alisema walikuwa wakutane kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi kujadili pamoja na mambo mengine, suala hilo...
“Kwanza nisiseme sana, maana ndiyo tunaingia kwenye Kamati ya Uongozi, nitafuteni baada ya kikao nitawaelezeni.”
Katika kipindi cha asubuhi, Sitta alisikika akiwataka wajumbe watoe hofu kuhusu dukuduku la Muungano kwa kuwa watapata fursa ya kuchangia mjadala kwa wiki nzima bila kufafanua kama itabidi kanuni itenguliwe au la.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 33(7) ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba za mwaka 2014, baada ya taarifa za kamati hizo kuwasilishwa, zitajadiliwa katika kipindi kisichozidi siku tatu.
Sitta katika kipindi hicho cha asubuhi, alisema kila siku watachangia wajumbe 50 na kila mmoja atatumia dakika 10 na kwa kuanzia, hiyo jana wajumbe 25 walitarajiwa kupata fursa ya kuchangia.

No comments:

Post a Comment