EBENEZA MARCH 9 2014

EBENEZA MARCH 9 2014

Wednesday, March 12, 2014

MARANDO AFUFUA TENA UPYAA KESI YA BABU SEA ASEMA ALIBAMBIKIWA NA UKWELI WOTE KUHUSU KESI HIYO NI HUU......

WAKILI maarufu nchini, Mabere Nyaucho Marando amesema mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na watoto wake watatu walimbambikiwa kesi.

Mabere Nyaucho Marando akiongea na waandishi wa Global Publishers (hawapo pichani).
Akizungumza na waandishi wa habari wa Global Publishers katika ofisi zao zilizopo Mwenge Bamaga mwishoni mwa wiki iliyopita, Marando alisema alipitia jalada la kesi hiyo lenye kurasa 1,362 na kugundua kuwa hakuna hata sehemu moja inayomhusisha kigogo mmoja wa nchi, lakini kesi walikuwa wamebambikiwa.
Hakutaja waliombambikia. Baadhi ya mahojiano ya Marando na waandishi wetu yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwandishi: Wewe uliwatetea Babu Seya na watoto wake, unaweza kutueleza ilikuwaje ukatafutwa wewe kuwatetea?

Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.
Marando: Kuna rafiki yangu alikuja kuniomba nifanye kazi ile, nilikataa hasa kwa kuwa nami nina watoto wa kike. Baadaye nilikubali kwanza kusoma jalada la kesi lenye kurasa 1,362 nikaona hawakufanya makosa waliyoshitakiwa, walibambikiwa nikaamua kuwatetea katika ngazi ya rufaa, niliwatetea bure kabisa.
Mwandishi: Kama hivyo ndivyo, ina maana makosa walibambikiwa?

Marando: Ndiyo, naamini makosa yale walibambikiwa lakini siyo na kigogo yeyote wa serikali katika nchi hii. Lakini Mahakama ya Rufaa haina makosa, Babu Seya na wanawe walikuwa wamehukumiwa na magazeti. Nyinyi waandishi mlimhukumu kwa hii fabricated case (kesi ya kutunga) na sababu zipo.
Mwandishi: Je, kuna njia yoyote iliyobaki ya kumtoa Babu Seya na mwanaye?
Marando: Mimi kama wakili, hapo ndiyo mwisho wangu, nimenyoosha mikono. Nimeshindwa nusu, nimeshinda nusu (Kwa kuwatoa jela Mbangu na mdogo wake Francis Nguza na kubaki jela Nguza na Papii.)
Mwandishi: Umekuwa Chadema na kuna habari kuwa uliondolewa kuwa mwanasheria wa chama akapewa Tundu Lissu,pia kuna habari kuwa umekosana na mwenyekiti wako, Freeman Mbowe, Je,  kuna ukweli wowote juu ya hayo?
Marando: Sijawahi kuwa mwanasheria wa Chadema isipokuwa wanapokuwa na tatizo la kisheria huwa nawapa ushauri wakihitaji. Mheshimiwa Mbowe sijakosana naye isipokuwa katika vikao tunaweza kutofautiana na hivyo ndivyo chama makini kilivyo. Wote hamuwezi kuwa na wazo moja katika hoja, baadaye inapigwa kura, upande unaoshinda na unaoshindwa huwa kitu kimoja. Hakuna ugomvi hapo, mimi ni Makamu  Mwenyekiti Kanda ya Pwani na Mjumbe wa Kamati Kuu.
Mwandishi: Lipo suala kuwa wewe ni usalama wa taifa na ulihusika na mauaji ya Komandoo Tamim, Je, hilo unaweza kulifafanua?
Marando: Mimi nilijiunga na usalama wa taifa na nilikuwa kitengo cha mambo ya nje hasa kuhusu vyama vya ukombozi enzi hizo. Niliacha kazi hiyo kwa kukabidhi barua kwa aliyekuwa mkurugenzi wake, Dk. Hansy Kitime baada ya kulazimishwa kujiunga na TANU kwani sikuwa mwanachama. Kuhusu Tamim aliuawa mwaka 1983 wakati huo mimi nilikuwa nimeshaacha kazi.
Hili la kuua walikuwa wakinipakazia watu wa usalama wa taifa bila shaka kwa sababu niliacha kazi kijeuri nikawa jobless (sina kazi).
Baadaye nikaajiriwa Shirika la Sheria Tanzania kabla ya kuanzisha kampuni yangu ya uwakili mwaka 1984. Nimefafanua hili mara nyingi sana, nadhani leo mmenielewa na Watanzania watanielewa.

No comments:

Post a Comment